1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

65 wajeruhiwa Afghanistan

Lilian Mtono
1 Julai 2019

Takriban watu 65 wamejeruhiwa katika shambulizi baya linalodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Taliban mashariki mwa mji wa Kabul. Shambulizi hilo lilifuatiwa na makabiliano kati ya wanamgambo na vikosi maalumu.

https://p.dw.com/p/3LOY8
Afghanistan Explosion in Kabul
Picha: picture-alliance/dpa/AP/R. Gul

Shambulizi hilo la bomu lililotegwa kwenye gari lililofanywa katika muda ambao huwa na shughuli nyingi lilisababisha moshi mzito katika eneo la Puli Mahmood Khan mjini Kabul na kutikisa majengo yaliyo hadi umbali wa kilomita 2 kutoka mahala palipofanyika shambulizi hilo. Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP alisema alisikia milio ya risasi baada ya mripuko wa bomu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan Nasrat Rahimi amesema, shambulizi hilo lilianza kwa washambuliaji kuripua bomu lililotegwa kwenye gari na baadaye washambuliaji kulizingira jengo. Hata hivyo vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwakabili washambuliaji hao.

Msemaji wa wizara ya afya Wahidullah Mayar, ameandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba miongoni mwa majeruhi hao 65 ni watoto tisa, huku akionya kwamba idadi huenda ikaongezeka.

Mmoja wa majeruhi Hedi Mohammad aliyekuwa akipata matibabu katika wodi ya dharura kwenye hospitali ya Wazir Akbar Khan alisema, "Kulikuwa na giza kila mahali, tukajificha ndani ya gari, kukawa na miripuko mingine miwili. Baada ya muda mwanga ukarejea ndipo wakatuchukua kutupeleka hospitali"

Afghanistan Explosion in Kabul
Baadhi ya majeruhi wameendelea kupata matibabu katika vituo vya afya Picha: Reuters/M. Ismail

Kuna nafasi gani ya kuendelea kwa mazungumzo ya Doha?

Msemaji wa wanamgambo hao Zabiullah Mujahid amechapisha taarifa inayosema wanamgambo hao walilenga eneo lenye majengo ya wizara ya ulinzi, ambalo lilizingirwa mara moja na vikosi vya usalama vya Afghanistan pamoja na magari ya huduma za dharura pamoja na helikopta.

Hata hivyo, mamlaka hazijathibitisha eneo halisi lililolengwa. Eneo jirani lililo na ulinzi mkali lina majengo yenye ofisi za idara ya kijasusi ya Afghanistan, wizara ya ulinzi, pamoja na shirikisho la soka la nchi hiyo na bodi ya mchezo wa kriketi. 

Msemaji wa shirikisho hilo la soka Shams Amini ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, shambulizi hilo lilifanyika karibu na lango kuu la makao makuu ya shirikisho, na baadhi ya watumishi wake bado wamenasa ndani ya jengo hilo.

Wanamgambo wa Taliban wamedai kufanya shambulizi hilo, siku mbili tu baada ya kuanza kwa raundi ya saba ya mazungumzo ya amani na Marekani huko Qatar, katika wakati ambapo Washington ikiwa na matarajio ya kupatikana kwa suluhu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais nchini Afghanistan mwezi Septemba.

Hakuna taarifa yoyote kutoka Doha iwapo mazungumzo hayo yataendelea hata baada ya mashambulizi hayo ama la. Mazungumzo hayo yanalenga masuala nyeti kuhusu vita dhidi ya ugaidi, uwepo wa vikosi vya nje nchini Afghanistan, mazungumzo yatakayohusisha makundi ya ndani yanayohasimiana na usitishwaji wa kudumu wa mapigano.