Zuma ataka mazungumzo kuhusu Libya yaanze haraka | Matukio ya Afrika | DW | 05.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Zuma ataka mazungumzo kuhusu Libya yaanze haraka

Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma ametoa wito kwa pande zinazohusika katika mzozo wa Libya kuanza haraka majadiliano ya amani. Ameyasema hayo baada ya mazungumzo na rais wa Urusi Dmitry Medvedev.

default

Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini amehimiza majadiliano ya amani yaanze haraka Libya.

Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma ametoa wito leo kwa Libya kuanza haraka majadiliano ya amani , baada ya mazungumzo yake na rais wa Urusi Dmitry Medvedev pembezoni mwa mkutano wa NATO.

Rais Jacob Zuma amesema leo kuwa katika mazungumzo yake na rais wa Urusi wamesisitiza haja ya kuanza mazungumzo haraka, na wameiomba NATO kusaidia kulishawishi baraza la taifa la mpito la waasi , kuondoa baadhi ya masharti ambayo yanakwamisha kuanza hatua hizo za mazungumzo. Zuma ni sehemu ya kundi kinachoongoza juhudi za umoja wa Afrika kusukuma mpango wa mataifa hayo wa amani ili kumaliza mzozo huo nchini Libya, mpango ambao hadi sasa umekataliwa na waasi, ambao wanasisitiza kuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ni lazima kwanza aondoke madarakani.

Mpango huo wa umoja wa Afrika , unatoa wito kwa pande zote katika mzozo wa Libya kufanya mazungumzo na kutayarishwa kwa jeshi la kimataifa la kulinda amani litakaloundwa na umoja wa mataifa ili kuangalia usitishaji wa mapigano. Wakati wa ziara yake mjini Sochi, Zuma pia alikutana na katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen, ambaye alikuwapo mjini humo kwa ajili ya mkutano wa baraza la majadiliano kati ya NATO na Urusi. Zuma amesema kuwa amefurahishwa na ukweli kwamba rais Medvedev ametoa uhakikisho wa nchi yake kuunga mkono mpango wa umoja wa Afrika. Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini Maite Nkoana-Mashabane amesisitiza msimamo wa umoja wa Afrika jana kuhusu suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Libya.

Zweiter Petersberger Klimadialog Axica Kongress- und Tageszentrum Berlin

Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini Maite Nkoana-Mashabane

Katibu mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen anatarajiwa kukutana na wajumbe wa upinzani wa Libya mjini Brussels wiki ijayo. Mkutano huo uliotishwa na Rasmussen umekubaliwa na mabalozi wa nchi 28 wanachama wa NATO na utafanyika Julai 13.

Ungarn NATO Außenministertreffen in Gödöllö Anders Fogh Rasmussen

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen atakutana na waasi mjini Brussels wiki ijayo.

Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Libya amekana kuwa serikali yake inafanya mazungumzo na waasi juu ya Muammar Gaddafi kuachia madaraka. Taarifa juu ya majadiliano kuhusiana na kung'atuka Gaddafi, ama kutafuta mahali salama pa kuishi ndani au nje ya nchi si sahihi, Moussa Ibrahim msemaji wa serikali ameliambia shirika la habari la reuters.

Gaddafi sio suala la kujadiliwa, huu ndio msimamo wetu wa msingi, na hali ya baadaye la Libya itaamuliwa na Walibya wenyewe. Gaddafi ni alama ya kihistoria na Walibya watakufa wakimtetea, amesema Ibrahim.

Ameongeza kuwa mazungumzo yaliyofanyika yanahusiana na usitishaji mapigano, misaada ya kiutu, na kuanza kwa majadiliano baina ya Walibya, na kisha hatua ya nne ambayo ni hatua ya mpito kuhusiana na mabadiliko ya kisiasa, hayo yataamuliwa na Walibya wenyewe.

Na Ufaransa imesema leo kuwa , waasi wanaopigana dhidi ya majeshi ya Muammar Gaddafi hawahitaji tena nchi hiyo , kuwadondoshea silaha, kwa kuwa hivi sasa wana uwezo mkubwa wa kujiongoza na wanaweza kupanga upatikanaji wa silaha wao binafsi.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/ rtre

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman

 • Tarehe 05.07.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11pKj
 • Tarehe 05.07.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11pKj