1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashtaka dhidi ya Zuma kufufuliwa upya

Saumu Mwasimba
16 Machi 2018

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anapaswa kusimama kizimbani kujibu mashtaka katika sakata ya muda mrefu ya kisheria inayomuandama kuhusiana na kupokea rushwa katika kadhia kubwa ya silaha.

https://p.dw.com/p/2uT9c
Südafrika Jacob Zuma
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/A. Ufumeli

Uamuzi huo umetangazwa na mamlaka ya kitaifa  inayohusika na kufungua mashtaka (NPA).Kesi hiyo ni ya muda mrefu toka 1999 wakati Zuma ambaye kipindi hicho alikuwa makamu wa rais alisimamia mpango huo wa biashara ya silaha wa mabilioni ya dola na kampuni moja ya Ufaransa.

Mnamo mwaka 2007 Zuma alishtakiwa kwa makosa 16 ikiwemo kupanga wizi,ufisadi,utakatishaji wa fedha pamoja na uhalifu wa kujipatia fedha kinyume cha sheria.Mashtaka yote yalitupiliwa mbali kabla ya kuingia madarakani kama rais mwaka 2009.

Baada ya miaka kadhaa ya changamoto za kisheria mahakama kuu nchini Afrika Kusini ikaamua mnamo mwezi Oktoba kwamba mashtaka  hayo yanaweza kufufuliwa tena hatua ambayo ilifungua njia leo Ijumaa ya kutolewa uamuzi huo wa mamlaka ya waendesha mashtaka wa serikali NPA.

Südafrika | Präsident Zuma tritt zurück ARCHIV
Waafrika Kusini wakishinikiza kuondolewa Zuma 2016Picha: Reuters/M. Hutchings

Kipindi cha utawala wake Zuma kiligubikwa na kadhia chungumzima za ufisadi zilizomfanya mwezi uliopita kuondoka madarakani mwezi uliopita kwa kulazimishwa kujiuzulu. Kwa muda mrefu Zuma amekuwa akidai kwamba mashtaka yanayomuandama yamechochewa kisiasa na kupikwa na kikundi cha watu wasiomkubali ndani ya chama tawala cha African National Congress ANC ambacho kilimuunga mkono aliyewahi kuwa rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki.

Akizungumza mbele ya waandishi habari Shaun Abraham mwendesha mashataka mkuu wa serikali kutoka mamlaka ya NPA amesema kwamba kwa maslahi ya uwazi na utawala unaozingatia haki pamoja na maslahi ya chombo hicho,mwelekeo bora kwa maoni yake ni kwamba mahakama ndiyo itakayokuwa jukwaa mwafaka la kutatua masuala haya na hatimae kufikiwa maamuzi.

Jacob Zuma ameshtakiwa kwa ufisadi unaohusika na biashara ya silaha ya serikali iliyogharimu dolla bilioni 2.5,katika kile ambacho kimeonekana kuwa uamuzi wa kipekee wa mahakama katika bara ambalo vigogo wa kisiasa ni nadra kuwaona wakikabiliana na siku kama hii mahakamani.

Hata hivyo Zuma mwenye umri wa miaka 75 ameyakanusha mashtaka yote yanayomkabili.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga