1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zilzala na juhudi za kuwaokoa wakaazi wa Haiti

Oumilkher Hamidou18 Januari 2010

Zilzala itumike kama fursa mpya ya kuikwamua Haiti na hali ya maskini,rushwa na matumizi ya nguvu

https://p.dw.com/p/LYld
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Clinton na rais wa Haiti Preval (kutoka kushoto)Picha: AP

Hali nchini Haiti, na mkutano wa wakuu wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze lakini na Haiti ambako zilzala kubwa kabisa iliyopiga katika nchi hiyo ya bahari ya Caribian imevuruga mfumo mzima wa kimaisha.Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:

"Mashirika ya misaada yamezidiwa kwa namna ambayo bila ya juhudi kubwa za wamarekani,hakuna chochote kinachoweza kufanyika.Na bila ya mchango wa muda mrefu wa Washington,Haiti pia haiwezi kua na mustakbal mwema.Mwito kama huo wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton hautatafsiriwa na wahaiti kama kitisho,bali njia ya kujitoa katika dhiki.Na pengine pia kama nia ya kutaka kufidia yaliyotokea zamani.Hili ni funzo linalotokana na kupuuzwa taifa dhaifu,hasa kama ni jirani

Gazeti la AUGSBURGER ALLGEMEINE linahisi pengine hii ni fursa njema kwa Haiti kujikwamua:Gazeti linaendelea kuandika

Pengine msiba huu utafungua njia kwa Haiti kujikwamua na kubuniwa pia utaratibu mpya wa misaada ya maendeleo.Kwasasa,wahaiti wanahitaji kila aina ya msaada wanaoweza kuupata.Kwa mtazamo wa muda mrefu lakini,watu watabidi watafakari vipi Haiti inaweza kusaidiwa vyema na kwa muda mrefu.Miradi chungu nzima ya ghali iliyoanzishwa miaka ya nyuma imegeuka magofu-kama haiti yenyewe ilivyoteketea."

Gazeti la BADISCHE ZEITUNG linazungumzia juhudi za kusambaza misaada na kuandika:

"Juhudi za Umoja wa mataifa ni za kushukuriwa.Hata hivyo wamarekani pia wanastahiki kushukuriwa:Wao ndio wenye helikopta za kutosha kuwafikia wahanga wanaoishi maeneo ya mbali ya Haiti-wao ndio wenye wanajeshi wa kutosha wanaodhamini usalama katika ujwanja wa ndege na katika kugawa misaada.Si suala la ubwana hili, pengine ni suala la kutaka kufidia miongo kadhaa ya kutoitilia maanani nchi hiyo.Kwa namna hiyo,Marekani haipaswi hata kidogo kuregeza kamba,hata kishindo cha zilzala kitakapopungua.Zilzala imefichua udhaifu wa Haiti ;Jukumu kubwa zaidi lililoko ni kuisaidia Haiti ijikwamue toka hali ya umaskini,rushwa na matumizi ya nguvu.

Jahresrückblick 2009 Wiederwahl von Angela Merkel
Mkuu wa chama cha kiliberali Guido Westerwelle akimpongeza kansela Angela Merkel baada ya kuidhinishwa October 28 iliyopita katika bunge la shirikisho mjini BerlinPicha: AP

Mada yetu ya pili na ya mwisho inahusu mkutano wa wakuu wa vyama vitatu vinavyounda serikali kuu ya Muungano mjini Berlin.Lengo la mkutano huo ni kumaliza mivutano kati yao.Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linaandika:

"Kimoja ni dhahir;Mkutano huo wa kilele ulioitishwa katika ofisi ya kansela haujasaidia kumaliza mivutano.Mkutano huo wa saa mbili na nusu kati ya wakuu wa vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali FDP,ulikua mfupi mno,hata kama ulimalizikia kwa chakula cha usiku.Pengine utasaidia kidogo kuleta hali ya kirafiki-ingawa hata hilo halina uhakika.Muhimu zaidi ni tofauti zilizopo katika sera za kodi ya mapato na mfumo wa afya..Tofauti hizo zimesalia pale pale hata baada ya mkutano huo wa kilele katika ofisi ya kansela.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir (Inlandspresse)

Imepitiwa na :Othman Miraji