1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Trump Asia na mabadiliko ya tabia nchi ,magazetini

Oumilkheir Hamidou
13 Novemba 2017

Ziara ya rais wa Marekani barani Asia, mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Bonn na mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano mjini Berlin ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini

https://p.dw.com/p/2nVw7
China Peking Xi Jinping und Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Tunaanza na ziara ya rais wa Marekani barani Asia ambako alihudhuria mkutano ya jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Asia na Pacific  APEC mjini nchini Da Nang nchini Vietnam.Trump hakubadilisha msimamo wake wa kutanguliza mbele masilahi ya Marekani, linaandika gazeti la Stuttgarter Nachrichten: "Ziara ya Trump katika eneo la mashariki na kusini mashariki ya Asia imedhihirisha: hata huko ametanguliza mbele masilahi ya kiuchumi ya Marekani tu. Makubaliano bora zaidi ya biashara ya dunia, watu wasiyategemee kutoka kwake.Trump anatembelea kwa wakati huu nchi ambazo sio tu zimeupakata utandawazi, bali pia zimeukuza. Lakini badala ya kuzungumzia utandawazi na ubinaadam, anaendeleza makosa ya miongo iliyopita. Ingawa anatilia mkazo azma ya kuimarisha nafasi za kazi Marekani na kufikia "makubaliano bora zaidi" siku za mbele, lakini sera zake hazionyeshi ishara ya kubuni nafasi bora zaidi za kazi nchini Marekani seuze kuchangia kurahisisha masharti bora zaidi ya kazi katika mataifa ya Asia yaliyoendelea kiviwanda."

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ya pwaya

Mazungumzo ya mabadiliko ya tabia nchi yameingia wiki yake ya pili mjini Bonn. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanahisi wiki ya kwanza ilipwaya, hakuna makubwa yaliyofikiwa. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Mkutano wa hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi haujagonga vichwa vya habari hadi wakati huu. Pengine hata katika wiki hii ya pili hali haitakuwa nyengine. Zoezi la jadi la kufika mikutanoni, viongozi wa taifa na serikali , nalo pia halitabadilisha pakubwa. Hali hiyo inasikitisha. "

Mazungumzo ya kuunda serikali kuu yanazorota

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na  shaka shaka kama juhudi za  kuutathmini uwezekano wa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vinne, CDU/CSU, FDP na walinzi wa mazingira die Grüne nchini Ujerumani, zitafanikiwa. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika: "Suala muhimu watu wanalobidi kujiuliza ni kama  viongozi wa vyama wanaweza kuleta hali ya kuaminiana. Bila ya kujali maridhiano ya aina gani watafikia, kwanza wanabidi waahidi watafanya kila liwezekano kwa masilahi ya nchi hii na kwa kipindi cha miaka minne inayokuja. Ushirikiano ndio neno linalobidi kutuliwa mkazo . La sivyo bora waachilie mbali. Mivutano isiyokwisha au mfarakano si bora kuliko uchaguzi mpya.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman