1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zawadi ya amani ya Nobel kwa Obama

Miraji Othman9 Oktoba 2009

Barack Obama, mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel

https://p.dw.com/p/K2uK
Rais Barack Obama wa Marekani akitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Kairo,Misri, katikati ya mwaka huu, ambapo alitoa mwito wa kuweko ushirikiano mpya baina ya nchi yake na Ulimwengu wa KiislamuPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani leo ametangazwa kwamba ameshinda kutunukiwa zawadi ya amani ya Nobel kutokana na miito yake ya kutaka ipunguzwe mirundiko ya silaha za kinyukliya na kufanya kazi kwa ajili ya amani ya dunia. Akiwa ni Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika kukamata wadhifa wa juu kabisa katika nchi yake, Barack Obama ametoa mwito wa kupunguzwa silaha na amejitahidi tangu alipokamata madaraka uanzishwe tena mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati ambao umekwama. Zawadi hiyo ilio ya kitita cha dola milioni 1.4 atakabidhiwa Barack Obama hapo Disemba 10 mjini Oslo.

Saa moja iliopita,Thorbjorn Jagland, mwenyekiti wa Kamati ya zawadi ya amani ya Nobel huko Norway alisema Barack Obama ameshinda zawadi hiyo kwa mwaka huu wa 2009 kutokana na juhudi zisizokuwa za kawaida katika kuimarisha diplomasia ya kimataifa na ushirikiano miongoni mwa wananadamu. Kamati hiyo imesema ni nadra kwa mtu wa kiwango kama kile cha Obama kuivutia dunia na kuwapa watu wa dunia hii matumaini ya mustakbali ulio bora.

Jina la Barack Obama lilitajwa katika tetesi kwamba huenda akatunukiwa zawadi hiyo, lakini wachunguzi wengi wa masuala haya ya zawadi ya Nobel waliamini kwamba ilikuwa mapema mno kwa rais huyo kutunukiwa zawadi hiyo kwa sasa. Kwamba ameipata zawadi hiyo ikiwa ni miezi tisa tu tangu awe rais ni mshangao mkubwa.

Kamati hiyo ya Nobel ilisema iliwekea umuhimu maalum juu ya fikra na kazi ya Obama katika kutaka kuwa na dunia isiokuwa na silaha za kinyukliya. Ilisema Obama, kama rais, ameunda hali mpya katika siasa ya kimataifa, na kwamba diplomasia ya kimataifa imerejea tena katika mahala pa katikati, uzito ukiwekewa katika mchango unaoweza kutolewa na Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi nyingine za kimataifa.

Rais wa zamani wa Finnland, Martti Ahtisaari, ambaye alishinda zawadi hiyo ya amani ya Nobel mwaka jana, alikuwa na haya ya kusema punde alipopata habari ya kuchaguliwa Barack Obama kwa zawadi hiyo....

Martti Ahtisaari 2005
Martti Ahtisaari, rais wa zamani wa Finnland na mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel mwaka 2008Picha: AP

"Safari hii inaonesha wazi kwamba wanataka kumtia moyo Rais Obama kuendelea na masuala ambayo amekuwa akiyazungumza, na, kama vile mwenyekiti wa Tume ya Uteuzi alivosema, kwamba kamati hiyo imekuwa ikijaribu kuhamasisha sera za kimataifa kuhusu masuala yote ambayo Rais Obama amekuwa akiyashughulikia."

Naye mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel kutokea Kenya, Bibi Wangari Maathai, alisema haya:

Die Friedensnobelpreisträgerin Wangari Maathai aus Kenia
Mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, Wangari Maathai, kutoka KenyaPicha: AP

" Naweza tu kuwa na matumaini kuwa wakati Obama anaendelea kuwa nyota inayong'ara, Bara la Afrika linapata changamoto kuleta hali bora zaidi, na kusitisha mizozo ambayo tunayo katika Bara la Afrika, kupunguza umaskini na kutoa nafasi kwa Afrika kujionyesha kwa hali bora zaidi duniani, kama vile Obama anavyotoa changamoto kwao."

Lakini Barack Obama huko kwao bado anakabiliana na mitihani na bado inangojewa kuonekana kama ataipita mitihani hiyo katika siasa za ndani na nje. Mwezi Aprili, katika hotuba yake katika mji wa Prague, katika Jamhuri ya Cheki, Obama aliahidi kwamba Marekani inatafuta kuweko amani na usalama duniani bila ya kuweko silaha za kinyukliya. Pia alitaka zipunguzwe silaha duniani, na kutoa ahadi ya kuufufua mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati.

Mshauri mkuu wa amani kwa upande wa Wapalestina, Saeb Erekat, amekaribisha Obama kutunukiwa zaidi hiyo ya Nobel, na akasema wao wanataraji Obama ataipatia amani Mashariki ya Kati na Israel itarejea nyuma katika mipaka yake ya mwaka 1967, kwamba kutaundwa dola ya Kipalestina ndani ya mipaka ya mwaka 1967, mji wake mkuu ukiwa Jerusalem.

Obama ni Mmarekani wa pili kutunukiwa zawadi hiyo, akitanguliwa na makamo wa rais wa zamani, Al Gore, hapo mwaka 2007, na Jimmy Carter mwaka 2002.

Mwandishi:Othman Miraji /Reuters/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman