1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 700 wauwawa katika hija

Admin.WagnerD24 Septemba 2015

Mkanyagano mkubwa umeuwa takriban watu 717 na kujeruhi wengine mamia wakati wa ibada ya hija Saudi Arabia Alhamisi (24.09.2015) mojawapo ya maafa mabaya kabisa kutokea wakati Waislamu wakitekeleza ibada hiyo.

https://p.dw.com/p/1GdBA
Majeruhi wa mkanyagano wa hija huko Mina Saudi Arabia. (24.09.2015)
Majeruhi wa mkanyagano wa hija huko Mina Saudi Arabia. (24.09.2015)Picha: Reuters/Stringer

Mkanyagano huo ambao ni maafa ya pili kuwakumba muhujaji mwezi huu kufuatia kuanguka kwa winchi ya ujenzi katika mji mtakatifu wa Meccan umetokea wakati wa utaratibu wa kumpiga mawe shetani kwa ishara.

Miili ya mahujaji ikiwa na mavazi yao meupe ilikuwa imetawanyika pamoja na viatu,chupa za maji zilizo pondwa pondwa na miamvuli waliokuwa wakiitumia mahujaji hao kujikinga na jua.

Idara ya ulinzi wa raia imesema bado inaendelea kuhesabu maiti ikiwa ni pamoja na mahujaji kutoka nchi mbali mbali na kwamba watu 863 wamejeruhiwa katika mkanyagano huo.

Takriban watu milioni mbili kutoka duniani kote wanashiriki hija hiyo mmojawapo wa mkusanyiko mkubwa kabisa wa kila mwaka duniani.

Mahujaji walaumiwa kwa ajali

Iran imesema raia wake 43 wamekufa katika mkanyagano huo na imeishutumu Saudi Arabia kwa makosa ya usalama yaliosababisha ajali hiyo.

Mahujaji na wafanyakazi wa uokozi katika eneo la maafa Mina.(24.09.2015)
Mahujaji na wafanyakazi wa uokozi katika eneo la maafa Mina.(24.09.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo

Lakini waziri wa Saudia amewalaumu mahujaji wenyewe kwa kwa kusema kwamba hawakufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka za serikali.

Waziri wa Afya amekaririwa akisema mahujaji wamekuwa wanakwenda bila ya kuzingatia ratiba ya hija hiyo.Khalid al Falih akizungumza na kituo cha televisheni cha El- Ekhbariya amesema ingelikuwa mahujaji hao wamefuata maelekezo ajali ya aina hiyo ingeliweza kuepukwa na ameahidi kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi.

Mkanyagano huo umetokea saa tatu asubuhi muda mfupi baada ya idara ya ulinzi wa kiraia kusema kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba ilikuwa inashughulikia ajali ya msongamano wa watu huko Mina mji ulioko kama kilomita tano kutoka mji mtakatifu wa Mecca.

Utaratibu wa kumpiga mawe shetani

Mamia kwa maelfu ya mahujaji walikuwa wamekusanyika Mina leo hii kwa ajili ya kumpiga mawe shetani kwenye nguzo tatu zilizomithilishwa na shetani kwa ajili ya utaratibu wa mwisho wa ibada ya hija ambayo inamalizika rasmi hapo Jumapili.

Mahujaji wakimpiga mawe shetani Mina. (24.09.2015)
Mahujaji wakimpiga mawe shetani Mina. (24.09.2015)Picha: Getty Images/AFP/M. Al-Shaikh

Afisa mmoja wa hospitali ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ajali hiyo imetokea nje ya daraja la Jabarat ambapo utaratibu huo wa kumpiga mawe shetani hutekelezwa.

Afisa huyo amesema kundi la mahujaji lililokuwa likiondoka eneo hilo liligongana na kundi jengine lililokuwa linakwenda upande ule ule wanakotokea mahujaji waliokuwa wakiondoka au waliokuwa wamepiga kambi nje.

Ajali ya pili mwezi huu

Helikopta zilikuwa zikiruka angani na mkururo wa magari ya kubebea wagonjwa ulikuwa ukiwatowa mahujai waliokuwa kwenye machela.

Muhujaji wakielekea kumpiga mawe shetani Mina. (24.09.2015)
Muhujaji wakielekea kumpiga mawe shetani Mina. (24.09.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Elshamy

Ajali hiyo inakuja wakati Waislamu bilioni 1.5 duniani wakiadhimisha siku ya Eid el Adha au Id el Hajj siku muhimu kabisa katika kalenda ya Waislamu.

Hiyo ni ajali ya pili kwa mahujaji mwaka huu baada ya winchi ya ujenzi kuanguka hapo Septemba 11 katika msikiti mkuu katika mtakatifu wa Mecca na kuuwa watu 111 wakiwemo wageni wengi.

Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu na kila Muislamu mwenye uwezo anatakiwa aitekeleze angalu mara moja katika uhai wake.

Kwa miaka mingi hija imekuwa ikikabiliwa na majanga ya mkanyagano na moto lakini kwa takriban muongo mzima kumekuwa hakuna ajali kubwa za aina hiyo kufuatia hatua za kuboresha usalama.

Hapo mwaka 2006 mahujaji 364 waliuwawa katika mkanyagano wakati wa kumpiga mawe shetani.

Na hapo mwaka 1990 mkanyagano mkubwa katika njia ya chini ya ardhi huko Mina uliuwa mahujaji 1,426 baada ya kukosa pumzi wengi wao wakitokea Asia.

Mwandishi : Mohamed Dahman AFP

Mhariri :Iddi Ssessanga