1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yapasa kuingilia kati Syria,wasema wahariri

Abdu Said Mtullya14 Machi 2012

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya Syria , mgogoro wa madeni barani Ulaya na juu ya hatua ya kusimamisha mapambano Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/14KML
Mauaji yaendelea Syria
Mauaji yaendelea SyriaPicha: dapd

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linasema wakati sasa umefika wa kuuzima moto unaowaka nchini Syria. Mhariri wa gazeti hilo anasema mazingira ya kuiruhusu jumuiya ya kimataifa kuingilia kati nchini Syria yameshajitokeza.

Mhariri wa "Süddeutsche Zeitung" anatilia maanani katika maoni yake kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea nchini Syria na watu wanazidi kufa. Anasema, wakati ukatili unaendelea jambo moja halipo.! Uwezekano wa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuuzima moto.

Gazeti la "Märkische Allgemiene" linazungumzia juu ya hatua ya kusimamisha mapambano baina ya Israel na makundi ya wapiganaji wa Kipalestina. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mtazamo wa Misri juu ya Israel siku zote umekuwa wa pande mbili. Aliyekuwa mtawala wa muda mrefu nchini Misri Mubarak alifanya tahadhari juu ya hisia za chuki dhidi ya Israel miongoni mwa watu wake. Lakini Mubarak hakuitembelea Israel. Katika upande mwingine makamu wake Omar Suleiman alipendelea sana kufanya ziara nchini Israel. Kwa hivyo inawezekana kwamba Suleiman ametumia fursa ya uhusiano wake na Israel ili kusuluhisha baina ya nchi hiyo na wapiganaji wa Kipalestina.

Suleiman anatambua kwamba amani baina ya Israel na Wapalestina inaituluza mihemko na pia inaleta manufaa kwake kwani anakusudia kugombea urais wa Misri.

Gaezeti la "Stuttgarter Nachrichten" leo linauzungumzia mgogoro wa madeni barani Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anawataka viongozi wa Ulaya wachukue wajibu zaidi katika kuukabili mgogoro wa madeni. Mhariri huyo anasema hakuna kitabu chenye mwongozo unaoonyesha jinsi ya kulipa madeni. Na hakuna anaejua kwa uhakika nini cha kufanya katika Umoja wa nchi zenye viwango tofauti vya maendeleo ya uchumi. Hata viongozi wanatutusa kizani.! Wanachofanya ni kujaribu hili na lile, kugusa hapa na pale. Lakini kinachotakiwa sasa ni kwa wanasiasa kufanya juhudi kubwa katika kuutekeleza wajibu wao.

Mhariri wa "Straubinger Tagblatt" anawakosoa mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa sarafu ya Euro kwa kuiruhusu Uhispania kuendelea kuwa na nakisi kubwa mnamo mwaka huu vilevile. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mawaziri hao hawapaswi kushangaa ikiwa watu wanalalamika juu yao. Wameiruhusu Uhispania iendelee kuwa na pengo kubwa katika bajeti yake wakati ambapo nchi za Ulaya zimeazimia kuwa na sera ya pamoja juu ya nidhamu ya bajeti.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman