1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

YANGON: Mjumbe wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa awasili Myanmar

11 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CBJv

Mjumbe wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Paulo Sergio Pinheiro, amewasili nchini Myanmar kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Katika ziara yake ya siku tano, na ambayo pia ya kwanza katika kipindi cha miaka minne, mjumbe huyo atachunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi katika kuyazima maandamano ya kupigania demokrasia yaliyoongozwa na watawa wa kibuda mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva nchini Uswisi, wamesema Paulo Sergio Pinheiro amewasilisha orodha ya magereza na vituo vya kuwazuilia wafungwa anavyotaka kuvitembelea wakati wa ziara yake nchini Myanmar.

Ziara ya Paulo Sergio Pinheiro inafanyika siku mbili baada ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeushulikia mzozo wa Myanmar, Ibrahim Gambari, kuondoka mjini Yangon baada ya kufanya ziara ya siku sita.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Singapore, George Yeo, amesema ziara ya Ibrahim Gambar nchini Myanmar ilikuwa na mafanikio.

´Nadhani Gambari alifaulu katika ziara yake ya hivi karibuni. Hakufaulu sana kama wengi wetu tulivyotumai, lakini kulipatikana ufanisi fulani. Hakukutana na watu wote waliotaka kukutana nao, lakini alikutana na Aung San Suu Kyi.´

Ziara ya Ibrahim Gambari imeleta matumaini makubwa kwamba jeshi la Myanmar litakuwa tayari kushiriki kwenye mazungumzo juu ya mageuzi ya kisiasa pamoja na kiongozi wa upinzani nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi.