1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

YANGON : Maandamano ya dunia dhidi ya Myanmar

6 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Hy

Wanaharakati leo wamekuwa na maadamano ya dunia dhidi ya utawala wa kijeshi wa Myanmar baada ya utawala huo kukiri kuwashikilia mamia ya watawa wa kibuda wakati wanajeshi walipovunja kwa kutumia nguvu maandamano ya kudai demokrasia wiki iliopita.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International lenye makao yake mjini London Uingereza limeandaa maandamano hayo katika miji kadhaa ya Asia,Ulaya na Amerika ya Kaskazini kwa matumaini ya kutuma ujumbe kwa magenerali wa Myanmar kwamba dunia ingali bado inaangalia hali ya nchi hiyo.

Wakati mjumbe wa maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar Ibrahim Gambari ameuonya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo juu ya taathira nzito za kimataifa kutokana na ukandamizaji wao wa maandamano ya kudai demokrasia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anasema hali nchini humo bado ni ya wasi wasi.

Ban anasema hali kwa jumla bado inaendelea kuwa ya wasi wasi sana hususan kuhusiana na hatima isiojulikana ya idadi kubwa ya watu ambao wamekamatwa bila ya kufuata mchakato wa kisheria.

Maandamano dhidi ya serikali ya kijeshi ya Myanmar yamefanyika miongoni mwa miji mengine Bangkok nchini Thailand,Manila Ufilipino,Kuala Lumpur nchini Malaysia,London Uingereza,Australia na pia yalikuwa yamepangwa kufanyika nchini Austria,Ubelgiji,Ufaransa,Ujerumani, Ireland ,Uhispania Swirtzerland, Marekani na Canada.