1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyochambuliwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Oummilkheir7 Juni 2007

Mkutano wa kilele wa G8 mjini Heiligendamm na kongamano la kiinjili mjini Cologne ndizo mada za leo

https://p.dw.com/p/CHSl

Mkutano uliokua ukisubiriwa kwa hamu wa viongozi wa mataifa tajiri kiviwanda na Urusi-G8 umeanza hii leo mjini Heiligendamm,kaskazini mwa Ujerumani.Chini ya uongozi wa kansela Angela Merkel wa Ujerumani,viongozi wa taifa na serikali watajadiliana kwa muda wa siku tatu kuhusu mada tete mfano hifadhi ya hali ya hewa, na jinsi ya kuupiga vita umasikini katika nchi zinazoinukia.Ratiba hiyo nono ndio kiini cha uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo-sawa na kongamano la kanisa la kiinjili mjini Cologne.

Tuanze basi na mkutano wa kilele wa G8.Gazeti la BERLINER MORGENPOST linaandika:

Viongozi wa mataifa sabaa tajiri zaidi kiviwanda na Urusi-G8 wanabishana juu ya mada mbali mbali.Hali hiyo inaashiria malumbano na matumaini pia.Kitovu cha malumbano ni hifadhi ya hali ya hewa.Kumechomoza falsafa ya aina mbili upande huo hasa tangu rais George W. Bush alipozindukana na kutambua haja ya kuhifadhiwa hali ya hewa.Kwa vyovyote vile hayo ni mafanikio kuona kwamba hatimae waalimwengu wamezindukana na kutambua kwamba kuzidi hali ya ujoto duniani ni hatari kwa maumbile na mazingira.“

Gazeti la WESTFALENPOSTEN la mjini Hagen linaandika:

„Kuna hatari pengine patazuka maajabu,hasa mtu anapomsikia kansela Angela Merkel akiyataja yote yale yatakayojadiliwa mjini Heiligendamm:kuufanya utandawazi ujiambatanishe na mahitaji ya jamii,kuung’owa umasikini,uhuru wa kibiashara na kuwahimiza wawekezaji,bila ya kulisahau suala la kumaliza mizozo ya kimataifa….Wababe wanane wa dunia wanapokutana,watu hutegemea kuna yatakayofikiwa.Au vipi?Kwa vyovyote vile mwenyekiti wa G8-bibi Angela Merkel amewafanya watu wajiwekee matumaini hasa alipotamka kua hifadhi ya hali ya hewa ndio kipa umbele cha mkutano huu wa kilele.Walimwengu wameyatafsiri matamshi hayo kua ni sawa na kuahidi kumtanabahisha kiongozi mkakamavu wa Marekani George W. Bush akubali kuregeza kamba.“

Gazeti la mjini Cologne KÖLNISCHE RUNDSCHAU linaahisi:

„Kuna masuala ambayo mtu hawezi kuyajibu kijuu juu.Sera za hali ya hewa ya kimataifa ni miongoni mwa masuala hayo.Ndio maana ni muhimu na ni jambo linalostahili kusifiwa kwamba kansela Angela Merkel hakuchelea, si hivi sasa mkutano mkuu unapoanza na wala si kabla ya hapo,kuzungumzia kinaga ubaga mada hiyo hata kama Marekani itaudhika.Wala haimaanishi kwamba mkutano wa kilele utashindwa.Enzi za ahadi za kijuu juu za Marekani zimeshapita.“

Mada nyengine magazetini hii leo inahusu kongamano la kanisa mjini Cologne.Watu 50.000 walihudhuria misa ya ufunguzi ya hadhara hapo jana.Watu milioni moja wanatazamiwa kuhudhuria kongamano hilo la likiinjili litakaloendelea hadi jumapili ijayo.Na huko pia mada kuu ni kuhusu utandawazi.Gazeti la KÖLNWER STADT ANZEIGER linaandika:

„Makanisa yanajua vilivyo utandawazi ni nini.Visugudi vya kisiasa,ubeberu wa kitamaduni,na kutumiwa mno mali ghali kwa masilahi ya upande mmoja.Kwa hivyo si hasha kama kanisa litaliingilia suala hilo la utandawazi na kudai haki.“