Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo | Magazetini | DW | 15.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Makubaliano yanayoruhusu wageni waishi na pendekezo la Tony Blair ndizo mada zilizohodhi magazeti ya Ujerumani

Serikali kuu ya muungano imeunga mkono kimsingi haki ya kuishi humu nchini wageni wasiokua na kibali madhubuti .Familia ambayo wameshaishi kwa miaka sita,na watu wasiokua na familia wanaoishi tangu miaka minane iliyopita nchini Ujerumani wataruhusiwa kusalia ikiwa wataweza wenyewe kuhudumia maisha yao.Mada nyengine magazetini inahusu pendekezo la waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair la kubadilisha mkakati kuelekea eneo la mashariki ya kati.

Kuhusu suala la haki ya kuishi wageni humu nchini gazeti la FRÄNKISCHE la mjini Bamberg linaandika:

“Wanasiasa wa kutoka vyama ndugu vya CDU na CSU wamefanikiwa kuufanya msimamo wao mkali ukubaliwe wakati wa mazungumzo pamoja na washirika wao katika serikali kuu ya muungano..Ni msimamo mkali mno.Wawakilishi wa kanisa wanahofia kati ya wageni elfu kumi hadi elfu 30 wanaweza pengine kuruhusiwa kubakia.Na wengine wote watakaosalia pengine watarejeshwa makwao.Pasiwepo atakaefikiria wahusika wamebarikiwa.Kwasababu kila mmoja wao ,hata wasomi,wanafanya kila liwezekanalo kutafuta kazi ili kuzihudumia familia zao.Hata kama vizuwizi vya kisheria vinafanya iwe shida kwao kupata kazi.”

Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn linaandika:

„Makubaliano yaliyofikiwa yanaweka viunzi ili hasa kuzuwia kutumiwa vibaya huduma za jamii.Si rahisi hata kidogo kwa watu ambao si wajerumani kupata kazi katika soko la ajira ambalo tokea hapo limepwaya.Kwa hivyo bustani ya peponi haikutikani hata kidogo katika ardhi ya Ujerumani.Maridhiano yaliyofikiwa lakini yanachangia katika kuendelezwa kwa busara mijadala kuhusu wageni.Juhudi za kuwajumuisha wageni katika maisha ya kila siku ya jamii,zinaweza kusaidia kupunguza pengo linalotokana na kupungua idadi ya wakaazi wa Ujerumani.“

Gazeti la mjini Rostock- OSTSEE –Zeitung linaandika:

„Wageni wanaovumiliwa nchini Ujerumani wanaweza wakati wowote kurejeshwa makwao.Kwa jamii ya wahusika hali hiyo inaleta hofu-kwasababu sheria zinaruhusu.Ndio maana Umoja wa ulaya umetoa muongozo kushadidia haki ya kuishi wageni kuambatana na sheria.Kwa hivyo serikali kuu ya Ujerumani imebidi kusaka maridhiano.Ni kwa masilahi ya kimsingi ya raia wa Ujerumani,wageni watakapoambiwa kinaga ubaga kwamba humu nchini wenye uhakika wa kuishi bila ya shida ni wale tuu wenye kuaminika na ambao wako tayari kujiambatanisha na maisha ya kijamii ya humu nchini.“

Tuigeukie mada ya pili magazetini.Kutokana na kuzidi matumizi ya nguvu nchini Irak na kukwama utaratibu wa amani ya mashariki ya kati,waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair anataka mkakati ubadilishwe.Anapendekeza nchi ambazo hadi sasa zimekua zikitengwa na nchi za magharibi,Syria na Iran zihusishwe katika mijadala ya kuifumbua mizozo hiyo.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamelichambua kwa mapana na marefu pendekezo hilo.

Gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linahisi waziri mkuu wa Uengereza anafuata njia inayofaa.Gazeti linaendelea kuandika:

„Tony Blair anaonyesha kawapita akina Bush na Olmert.Pendekezo lake la kubuniwa mfumo wa aina mpya kudhamini usalama katika eneo zima la mizozo - mashariki ya kati,linamfanya mtu aamini kuna aliyezindukana na kutambua kwamba huwezi kuendelea daima kufumbia masikio madai ya wananchi wako mwenyewe.Hapa Tony Blair anafuata ule usemi asilia „fikiria mbali zaidi“,japo kama kwa kufanya hivyo analenga kurekebisha hadhi yake iliyochujuka.