1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

6 Julai 2005

Afrika katika mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda G8 na kashfa ya rushwa katika kampuni la magari ya Ujerumani Volkswagen ndizo mada zilizochambuliwa zaidi hii leo na magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHNT

Kuhusu mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda G8 na suala la Afrika,gazeti la Mitteldeutsche uzeitung la mjini halle linahisi:

„Fedha pekee hazisaidii barani Afrika.Watabidi wajiulize,njia ipi nyengine itumiwe.Kusamehewa mikopo na misaada ziada ifungamanishe na masharti kwa watakaofadhiliwa.Hakuna atakaebisha.Kenya kwa mfano haitekelezi masharti ya uwazi,kwac hivyo isifaidike na mpango wa kusamehewa madeni.Hakuna shaka yoyote,bila ya kudhaminiwa utawala bora,uhuru wa vyombo vya sheria, na sera madhubuti za kupambana na rushwa,hata mamilioni ziada yataingia katika makasha yale yale ya zamani na kuzidi kuwatajirisha matajiri wa zamani.Mwenye macho haambiwi tazama-hakuna anaeweza kubisha.

Gazeti la TAGESSPIEGEL la mjini Berlin linachambua matumaini yake kuelekea mkutano huo wa kilele wa G8 nchini Scottland,gazeti linaandika:

„Suala kama G8 inaambata na wakati katika zama hizi za utandawazi,linabidi lijibiwe kwa undani kabisa na sio kijuu juu.Na hapo ndipo unapokutikana umuhimu wa Gleneagles.Tony Blair, ambae ndie mwenyeji wa mkutano huo wa kilele,amefanikiwa kuorodhesha juu kabisa mada za Afrika na usafi wa hali ya hewa ajenda ya mkutano huo licha ya upinzani wa viongozi wenzake.Manung’uniko yamekua yakisikika hata miongon i mwa ujumbe wa Ujerumani watu wakihoji mkutano wa kilele wa kiuchumi ungebidi ujishughulishe kwanza na kupanda bei ya mafuta kwa mfano.Hilo ndilo litakalokua la mwanzo ,pakiwepo miito ya kuzidi uwazi katika masoko ya kimataifa na wakati huo huo kupunguza mitindo ya kubahatisha bahatisha katika masoko ya hisa.Pili hata baada ya kuchaguliwa upya, mada hizo moto moto hazijamuia rahisi Blair.Kuna haja ya kutolewa ufafanuzi,kwa mfano kama Afrika kweli inahitaji fedha zaidi kutoka nchi za magharibi au kama isingekua bora kufungua milango ya masoko kwa bidhaa kutoka Afrika.

Nalo gazeti la mjini LÜNEBURG linahisi:

„Misaada ya maendeleo iongezwe mara dufu,ndio mwito wa Bob Geldorf,muasisi wa tamasha ya Live 8 kwa viongozi wa mataifa manane tajiri kwa viwanda.Wanamuziki na wasanii kwa jumla wanauonya ulimwengu si jambo linalokubalika kuona kila sekondi tatu mtoto mmoja mdogo anakufa kutoka na umasikini barani Afrika.Ni kweli lakini pia si rahisi hivyo .Misaada inaliponza bara la Afrika.Misaada mara nyingi inaangukia mikononi mwa maafisa wanaokula hongo na sio wananchi wanaoihitaji.Waafrika wanazidi kupaza sauti kudai mageuzi.Nchi za magharibi zikiacha kuwaalipa wakulima wao fidia,zitakua zinasaidia zaidi kuliko kuwapatia nafaka.Ushuru wa forodha ukipunguzwa na vizuwizi vya kibiashara kuondoshwa,njia za kushindana kibiashara zitafunguka.Lakini wafadhili wanapendelea vyewngine.Matajiri wanataka kutakasa nyonyo zao kwa kutoa misaada mikubwa mikubwa,lakini wakati huo huo umasikini unaselelea.

Mada ya pili inahusu kashfa ya rushwa katika kampuni la magari la Volkswagen.Kashfa hiyo imezidi kukuza mijadala juu ya utaratibu wa kupitishwa maamuzi katika makampuni ya Ujerumani na kanuni za kampuni la magari la Volks Wagen.Wanasiasa na wataalamu wanazungumzia juu ya kufichuliwa siri za mishahara ya wawakilishi wa baraza la wafanyakazi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linaandika:

„VW lina mtindo wake wenyewe ambao hauambatani na uongozi wa kimambo leo seuze kukaguliwa.Pengine kampuni hilo limefura tangu lilipoingia katika daraja ya magari ya fakhari.Sio tuu linapohusika suala la safari za nje za viongozi wao na gharama za chakula,bali pia katika utengenezaji ambapo magari chapa PHAETON na BUGATTI hayalingani hata chembe na mahitaji sokoni-katika wakati ambapo gari la kawaida chapa ya VW hakuna mfanayakazi wa kawaida anaemudu kulinunua ,seuze tena hata umadhubuti wake unawekewa suala la kuuliza.Katika wakati ambapo wafanyakazi wanajiandaa kwa kipindi chengine cha kufunga mikaja,habari moto moto zinazidi kusikika jinsi mabosi wanavyomwaga fedha.Penye shida pana faraja.

Gazeti la WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN la mjini Münster limeandika:

„Mtindo wa VW ni wa aina pekee nchini Ujerumani.Na hali hiyo hiyo ya kipekee ndiyo iliyokua miaka nenda miaka rudi ikisifiwa na makundi yote ya kisiasa ya humu nchini.Sasa inadhihirika ufanisi si chochote si lolote.Hakuna kilichowagutua,na kila matatizo yanapochomoza bosi alijitokeza na mapendekezo mepya ya kufunga mikaja.Yadhihirika kana kwamba kampuni hilo limegeuka mtungi usiokua na tako.Lakini kabla ya chochote kufanywa itabidi kwanza utafiti wa kina kufanywa na kila mmoja kumulikwa.Hata kanuni za VW zitabidi zifanyiwe marekebisho.