1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyoandikwa magazetini hii leo

Oummilkheir16 Oktoba 2006

Vikwazo vya Umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya kaskazini na kuzidi umasikini nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/CHUh

Mada kuu magazetini hii leo nchini Ujerumani ni kuhusu vikwazo vilivyoamuliwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya kaskazini.Mbali na hayo wahariri wamezungumzia mipango ya wizara ya afya katika kupambana na maradhi ya kensa na kuzidi hali ya umasikini nchini Ujerumani.

Tuanze lakini na uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya kaskazini.Kwa mtazamo wa mhariri wa gazeti la NEUEN RUHR-ZEITUNG la mjini Essen vikwazo hivyo ni kichekesho.Gazeti linaandika:

“Korea ya kaskazini,nchi mojawapo masikini kabisa ya dunia,ambako hakuna anaesubutu kufurukuta, imewekewa marufuku ya watumishi kusafiri, ili kuwaadhibu kutokana na jaribio la kinuklea la nchi hiyo.Hata bidha za anasa hazairuhusiwi tena kuingia nchini humo.Na zaidi ya hayo wamekubaliana katika baraza la usalama Korea ya kaskazini isipatiwe tena teknolojia ya kinuklea.Kile ambacho mjini New-York kinasherehekewa kama ufanisi-kwasababu wote-hata China na Urusi- wameunga mkono azimio hilo ni kichekecho tuu.Baraza la Usalama la umoja wa mataifa halina msimamo mmoja-kwasababu pengo ni kubwa kati ya masilahi ya Marekani na yake ya jamhuri ya umma wa China.”Linaandika NEUEN RUHR ZEITUNG la mjini Essen.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine zeitung linaandika:

„Jibu la mwanzo la Pyongayang halionyeshi kama rais Kim Jong Il ataaridhia,ataona bora awaache maelfu ya raia wafe kwa njaa kuliko kuachana na miradi yake ya kinuklea.Lakini vizuwizi vya kibiashara-na hasa marufuku ya kupatiwa silaha-yanaweza kuidhoofisha serikali yake.Na kwa mara nyengine tena, majirani zake Urusi na China,ndio watakaoamua kama marufuku imara-au kiini macho tuu-linahisi gazeti la Frankfurter Allgemeine.

Frankfurter Rundschau linahisi vikwazo hivyo havitoshi.Maoni sawa na hayo yametolewa pia na gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linaloandika:

„ Hata kama Kognak na Kaviar vitakua haba-vikwazo hivyo havitamsumbua hata kidogo „kipenzi cha Korea ya kaskazini“ Kim Jong Il na majenerali wake.Ni Havina maana yoyote.Kizungumkuti ni kile kile :Washington na Tokyo wanataka kumbinya Kim Jong Il,China na Korea ya kusini wanataka mazungumzo yasivunjike.Mtindo huo wa kupigania masilani unaifanya hali katika eneo la mashariki ya Asia iwe ya hatari.

Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linahisi lawama zote zinazotolewa dhidi ya azimio la umopja wa mataifa,jee watu wamepima ili kuona kama kuna njia nyengine?Wangefanya nini?Watishie kuzusha vita.Au nchi hiyo ambako tokea hapo watu wanakufa kwa njaa na baridi,iwekewe vikwazo vikali vya kiuchumi ili izidi kuangamia.Ukweli ni kwamba hakuna ajuae vipi kukabiliana na kitisho kutoka Korea ya kaskazini.

Mada nyengine magazetini hii leo inahusu umasikini nchini Ujerumani.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linazungumzia juu ya ripoti iliyochapishwa kufuatia uchunguzi uliofanywa kwa niaba ya chama cha Social Democratic-kwa jina „Aina mpya ya umaskini“

Gazeti linaandika:

„Tabaka mpya ya chini inazidi kukua.Mikakati ya kueneza elimu katika miaka ya 70,pale malaki ya watoto wa familia za wasiojimudu walipokua wakisaidiwa kifedha ili wajiendeleze kimaisha,imesahauliwa.Ngazi imeondolewa-mradi wa kuhimiza maisha bora ya jamii umesitishwa,jamii nchini Ujerumani inabadilika na kuchukua muundo wa tabaka.

Nchini Ujerumani watu wanazungumzia juu ya dola lenye nguvu-panapohusika suala la usalama wa ndani.Kwa bahati mnbaya hakuna anaezungumzia juu ya dola le nye nguvu linapohusika suala la kuleta uwiano wa sera za jamii na zile za elimu.Kinachohitajika ni mkakati wa aina mpya utakaozingatia watoto,vijana,elimu na sera za jamii.“