1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna makubaliano ya kumpa kinga ya kutoshtakiwa Jammeh

22 Januari 2017

Viongozi wa mataifa ya Afrika magharibi hawakukubaliana kumpa kinga ya kutoshtakiwa Yahya Jammeh wakati wa mazungumzo yao ambayo yalimshawishi kukimbilia uhamishoni.

https://p.dw.com/p/2WDkY
Ex-Präsident Jammeh verlässt Gambia
Picha: Picture-Alliance/dpa/J. Delay

Jammeh ambaye anashutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, ameiongoza nchi yake kwa miaka 22 lakini alikataa kukubali kushindwa katika uchaguzi uliofanyika hapo mwezi wa Disemba. Ameondoka kwa ndege kutoka mji mkuu wa nchi Banjul hapo Jumamosi usiku wa manane wakati kikosi cha kanda hiyo kikiwa kinajiandaa kumuondowa kwa nguvu.

Kumalizika kwa amani kwa mkwamo huo kutamuwezesha kiongozi wa upinzani Adama Barrow ambaye aliapishwa kama Rais wa Gambia kwenye ubalozi wa Gambia katika nchi jirani ya Senegal hapo Alhamisi kushika madaraka.

Uamuzi wa Jammeh kun'gatuka umezusha tetesi juu ya masharti waliokubaliana wakati wa mazungumzo yao ya siku mbili yaliyoongozwa na Rais Alpha Conde wa Guinea na Mohammed Ould Abdel Aziz wa Mauritania.

Hakupewa kinga ya kutoshtakiwa

Gambia Ex-Präsident Yahya Jammeh
Aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh.Picha: Picture-Alliance/Gambia State TV via AP

Waziri wa mambo ya nje wa Senegal Mankeur Ndiaye ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters, viongozi wa kanda hawakwenda mbali kukubali kumpa kinga ya kutoshtakiwa licha ya juhudi za Jammeh kutaka apatiwe kinga hiyo.

Rais Jammeh na timu yake walitaka kuidhinishwa kwa azimio na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ambalo litampa kiongozi huyo kila hakikisho, muhimu ikiwa ni kinga ya kutoshtakiwa.

"Azimio la aina hiyo halikusainiwa na yoyote " amesema waziri huyo wa mambo ya nje wa Senegal. Ametowa kauli hiyo baada ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuchapisha azimio la pamoja kutoka vyombo vitatu kwa dhamira ya kufikia suluhisho la amani kwa hali ya kisiasa nchini Gambia.

Katika azimio hilo, zimeahidi miongoni mwa mambo mengine haki za Jammeh kama raia, kiongozi wa chama na kiongozi wa zamani wa taifa, kuzuwiya kunyakuliwa kwa vitu anavyomiliki yeye mwenyewe na marafiki zake na kuhakikisha kwamba hatimae anaweza kurudi nchini Gambia. 

Ndiaye hakuupa umuhimu waraka wa aina hiyo. Amesema "nataka iwe wazi hakuna mkuu wa nchi wa jumuiya ya ECOWAS aliyehalalisha azimio hilo na kwamba Barrow hakujulishwa juu ya waraka huo kabla ya kuchapishwa kwake."

 

Wagambia wachoshwa na utawala wa Jammeh

Gambia Machtwechsel - Senegalesiche Truppen verlassen die Grenze
Magari ya kijeshi ya Senegal mpakani na Gambia. Picha: Getty Images/AFP/Seyllou

Kushindwa kwa Jammeh katika uchaguzi wa tarehe Mosi Disemba na kukubali kwake awali kwa matokeo hayo kulisherekewa nchini kote na Wagambia ambao wamechoshwa na utawala wake unaozidi kuwa wa mabavu.

Lakini alibatilisha uamuzi huo wiki moja baadae na kuzusha mzozo na majirani zake wa kanda walioshinikiza ajiuzulu.

Mashirika ya haki za biinaadamu yanamshutumu kwa kuwafunga gerezani, kuwatesa na kuwauwa wapinzani wake wa kisiasa wakati mwenyewe akijipatia utajiri mkubwa yakiwemo magari ya kifahari na majumba nchini Marekani huku takriban watu wake wengi wakiendelea kuzama kwenye umaskini.

Jammeh ameondoka kwa ndege kuelekea Guinea ya Ikweta akisimama kwa muda katika mji mkuu wa Guinea, Conakry.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Lilian Mtono