1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wulff aagwa kwa gwaride la heshima

Rais wa Ujerumani aliyejiuzulu, Christian Wulff, aliagwa kwa heshima jana usiku katika uwanja wa kasri la rais la Bellevue. Mamia ya watu walifika karibu na uwanja huo kuandamana na kupiga kelele kwenye sherehe hiyo.

Wulff na mkewe Bettina

Wullf na mkewe Bettina

Sherehe za kumwaga Christian Wulff kwa gwaride la heshima ziligubikwa na kelele za mamia ya waandamanaji waliokusanyika nje ya uwanja wa kasri la Bellevue. Waandamanaji hao walikuwa wamebeba filimbi na tarumbeta aina ya vuvuzela na walipiga kelele kwa nguvu sana.

Sura ya Christian Wulff ilionyesha kwamba alikuwa amekasirishwa na kelele hizo zilizokuwa kama zile zinazopigwa kwenye uwanja wa mpira wa miguu. Gwaride la heshima alilopigiwa Wulff na wanajeshi wa Ujerumani lilichukua takriban dakika 40.

Waandamanaji nje ya uwanja wa kasri la Bellevue

Waandamanaji nje ya uwanja wa kasri la Bellevue

Miongoni mwa waliohudhuria sherehe za kumwaga Wulff walikuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Horst Seehofer anayeshikilia wadhifa wa urais kwa muda pamoja na wawakilishi wengine wa serikali ya Ujerumani.

Wanasiasa wasusia mwaliko

Marais wastaafu wote walikuwa wamealikwa lakini hakuna hata mmoja aliyehudhuria. Viongozi wengine ambao pia hawakuhudhuria ni makamu wa rais wa bunge la Ujerumani pamoja na rais wa mahakama ya katiba. Wanasiasa kutoka vyama pinzani vya Social Democratic Party (SPD), chama cha wanamazingira Die Grünen pamoja na chama cha mrengo wa kushoto Die Linken pia hawakuhudhuria. Hivyo jumla ya idadi ya watu waliofika kumuaga Wulff ilkuwa 200 ingawa wageni 370 walikuwa wamealikwa.

Wanajeshi wakipiga gwaride

Wanajeshi wakipiga gwaride

Kwa kawaida hakuna hotuba zinazotolewa katika hafla ya kumwaga mwanasiasa kwa gwaride la heshima. Anayeagwa anapewa nafasi ya kuchagua nyimbo tatu anazozipenda ambazo zitakazopigwa na bendi ya jeshi wakati wa sherehe. Miongoni mwa nyimbo alizochagua Christian Wulff ni wimbo wa "Somewhere over the rainbow."

Uchaguzi wa rais mpya wa Ujerumani utafanyika tarehe 18 mwezi huu. Hadi sasa hatma ya Christian Wulff na familia yake bado haijafahamika.

Mwandishi: Kay-Alexander Scholz

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 09.03.2012
 • Maneno muhimu wulff
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/14IIY
 • Tarehe 09.03.2012
 • Maneno muhimu wulff
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/14IIY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com