1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg ndio mabingwa wa DFB Pokal

4 Juni 2015

Wolfsburg walishinda kwa mara ya kwanza kabisa Kombe la Shirikisho la Kandanda Ujerumani - DFB Pokal, baada ya kuwabwaga Dortmund mabao matatu kwa moja katika fainali ilioyochezwa Berlin.

https://p.dw.com/p/1FbY0
Wolfsburg DFB-Pokal Autokorso Feier Benaglio
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Goli pekee la Dortmund lililoingizwa na mgabon Pierre Emerick Aubameyang lilifutiliwa mbali na magoli 3 ya haraka haraka yaliyoinginguzwa na Wolfsburg katika muda wa dakika 16 za kipindi cha kwanza, na kumpa kocha wa timu hiyo Dieter Hecking mwenye umri wa miaka 50, kombe lake la kwanza. Hilo pia lilikuwa kombe la pili katika historia ya klabu ya Wolfsburg katika historia yake, kombe jingine likiwa ubingwa wa ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga mwaka 2009.

Mdhamini mkuu wa Wolfsburg, kampuni maarufu ya magari ya Wolkswagen, iliandaa sherehe kubwa ya ushindi huo mjini Berlin, na kocha Hecking alisema kombe hilo ni jasho lao. ''Nadhani timu hii tayari inayo historia ndefu. Mimi nimekuwa kocha wake kwa miaka miwili na nusu, na mtu anapoweza kupata mafanikio, na kulibeba kombe, kwa kweli ni hali ya kufurahisha.''

Jürgen Klopp nimmt Abschied
Ulikuwa mchuano wa mwisho kwa Jürgen Klopp kama kocha wa DortmundPicha: Reuters/M. Sohn

Sherehe kwa Wolfsburg ilikuwa kilio kwa mpinzani wake Borussia Dortmund, ambayo iltarajia kumuaga kocha wake wa miaka 7 Jurgen Klopp kwa kombe hilo. Lakini haikuwa, badala yake Klopp ambaye alifurahiwa sana na klabu hiyo kabla ya kusuasua na kuaga msimu huu, aliagwa katika karamu isiyo na shamra shamra. Maneno yake ya kwa heri yaliakisi hali halisi katika klabu yake. ''Kama kipimo cha juhudi zetu kingechukuliwa kulingana na kupoteza mechi hii ya fainali, basi tusingeweza kupata mafanikio yaliyotufanya kuwa timu ambayo tumekuwa kwa miaka saba iliyopita. Nashukuru mafanikio hayo, lakini hayanipi faraja, kwa sababu katika hali hii faraja haiji kirahisi. Unapokuwa umepania sana ushindi, badala yake ukapata kipigo, inachukua muda kuweza kuyakubali.''

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu