1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg-mabingwa watamba mbele ya B.Moenchengladbach

19 Oktoba 2009

Hamburg na Leverkusen sare kileleni 0:0

https://p.dw.com/p/KAdF
C.Genter (Wolfsburg)Picha: picture-alliance / dpa

Chipukizi wa Ghana, chini ya umri wa miaka 20, waandika historia mwishoni mwa wiki waliporejea Accra na Kombe la Dunia-Je, hizo ni salamu za Afrika kabla ya kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika kusini ?

-Katika Bundesliga-mabingwa watetezi wa Ujerumani VFL Wolfsburg,wameparamia hadi nafasi ya 5 ya ngazi ya Ligi jana baada ya kuizaba Borussia Moenchengladbach mabao 2:1.

-Manchester United yaipiku Chelsea kileleni mwa Premier League baada ya kuitandika Bolton Wanderers mabao 2-1.

-FC Barcelona,mabingwa wa Spain, wako tayari kubadilishana stadi wao mfaransa Thiery Henry kwa mbrazil Robinho,anaechezea Manchester City.

-Na Brazil yaendelea kuongoza orodha ya dunia ya timu bora duniani mbele ya mabingwa wa Ulaya, Spain.

Mabingwa wa Ujerumani VFL Wolfsburg, kabla kurejea uwanjani kesho kwa changamoto za champions League nyumbani na Besiktas Istanbul,ilitamba jana nyumbani ilipoikomea Borussia Mönchengladbach inayoyumbayumba wakati huu mabao 2-1. Kwa ushindi huo, Wolfsburg imechupa hadi nafasi ya 5 ya ngazi ya Ligi.Edin Dzeko alipiga hodi mara 2 katika lango la Borussia na kukaribishwa ndani.

Mabingwa mara kadhaa Bayern Munich, nao wamerudia desturi yao ya kushinda.Munich iliitimu nje nyumbani mwao Freiburg kwa mabao 2-1 na hivyo kupanda hadi nafasi ya 6 ya ngazi ya ligi nyuma ya mabingwa Wolfsburg.Munich ina miadi kesho ya Champions League na wafaransa Girondins Bordeaux.

Msukosuko umeikumba Hertha Berlin,timu iliotia fora mno msimu uliopita tu na sasa imegeuka "alie juu ,mgonje chini". Berlin, ilizabwa mabao 3-0 na sasa imeun'gan'gania mkia wa Ligi haitaki kuutoa. Pigo la Berlin,limezidi kuwa kubwa kwavile, mpinzani wake mkiani FC Cologne, imeanza kujikomboa .Cologne ilitamba nyumbani kwa bao 1:0 dhidi ya Mainz.Frankfurt ikatoroka na pointi 3 kutoka Hannover.Schalke tayari Jumamosi, iliikomea Stuttgart mabao 2-1. Viongozi wa Ligi Hamburg walimudu sare nyumbani na mahasimu wao Leverksen 0:0.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Manchester United imeparamia kileleni kwa kuipiku Chelsea kwa pointi 1.Manu imeichapa Bolton Wandereres mabao 2:1.

Hii inafuatia Aston villa kutoka nyuma na kuibwaga Chelsea . Tottenham Hotspurs iko nafasi ya tatu nyuma ya Manu na Chelsea.Arsenal,ikiwa bado ina mchezo mmoja kucheza, imenyatia hadi pointi 4 kutoka kileleni kufuatia ushindi wake wa mabao 3-1 dhidi ya Birmingham City.

FC Barcelona , mabingwa wa Ligi ya Spian "La Liga" wako tayari kubadilisha na Manchester City: Robino-stadi wa Brazil kwa Thiery Henry wa Ufaransa.Taarifa zinasema kwamba,Barcelona haiko tayari kulipa kitita inachodai Manchester City cha Euro milioni 35.Barcelona inataka kuteremsha bei kwa kumtoa mhanga Henry, alieumia majuzi na abidi kupumzika kwa siku 10. Barcelona itayari kuipa Manchester City wachezaji kadhaa .Kati ya Robino na Barcelona, tayari kuna maafikiano.Robino anaielewa Ligi ya Spian barabara kwavile, amesha ichezea Real Madrid kati ya 2005 na 2008.Ni baadae, Robinho ,alipohamia Manchester City katika Premier League.

KOMBE LA DUNIA LA FIFA:

Brazil, inaendelea kuongoza katika orodha ya timu bora kabisa duniani ya FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni .Brazil imeipiku Spain, mabingwa wa Ulaya huku Holland ikifuata nafasi ya 3, mbele ya mabingwa wa dunia -itali, ilioanguka nafasi ya 4.Ujerumani imeteremka hadi nafasi ya 5,lakini mbele ya Argentina na Uingereza.Simba wa nyika-Kamerun imechupa nafasi 15 na kuangukia nafasi ya 14-ikiwa nafasi ya usoni kabisa kuchukuliwa na timu ya Afrika.

Kocha wa Argentina,Diego Armando Maradona, amesema hatataka radhi kwa maneno machafu ya utovu wa adabu aliotoa kwa maripota mapema wiki iliopita baada ya timu yake ya Argentina, kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia.

Hatahivyo, Maradona ,aliahidi amekubali kwa kadiri fulani, ila zilizotolewa kwa aliyoyasema. Maradona, aliahidi kwamba, hatasema tena alioyasema wala hatafanya tena aliofanya. FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni liliahidi kumpa adhabu Maradona kwa matusi yake ,licha ya kutaka radhi alao kwa akina mama.

TIMU YA GHANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 20 NI MABINGWA WA DUNIA:

Timu ya chipukizi ya Ghana,chini ya umri wa miaka 20, imekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutwaa kombe la dunia chini ya umri huo baada ya kuizaba Brazil, mabingwa mara 4 wa dunia mabao 4-3 katika changamoto za mikwaju ya penalty,mjini Cairo, ijumaa usiku.Ghana na Brazil , zilisimama sare 0:0 hata baada ya kurefushwa mchezo baada ya dakika 90.Ghana iliona mchezaji wake Daniel Addo, akitimuliwa nje ya uwanja na rifu na hivyo,kupindua juu chini mbinu ya mchezo ya waghana.

Uwanja wa Taifa wa Cairo,ukisheheni mashabiki maalfu kadhaa pamoja na rais wa FIFA, Sepp Blatter, uliwaona chipukizi wa Ghana, wakitoa salamu kwa dunia kwamba, mwaka wa Afrika katika kombe la dunia 2010 ,umeanza kwa kishindo.Salamu hizo bila shaka zimefika Brazil,Itali,Ujerumani,Spain na hata Ufaransa-timu zinazopigiwa upatu kuweza kutoroka Johannesberg,Julai 11, mwakani na Kombe la dunia.

Hii ilikua finali ya 3 kwa Ghana na ikawa "halali mara tatu".Ghana kwahivyo, imekuwa timu ya kwanza nje ya Amerika kusini na Ulaya ,kutwaa Kombe hilo la dunia la umri chini ya miaka 20.

CHAMPIONS LEAGUE:

Kombe la klabu bingwa barani Ulaya linarudi uwanjani kesho na keshokutwa :Kati ya timu 3 za Ujerumani,moja -Stuttgart,itakuwa uwanjani kesho:Mabingwa Wolfsburg na mabingwa mara kadhaa wa Ulaya, Bayern Munich watakuwa uwanjani keshokutwa Jumatano.Kati ya hizo 3 ni moja tu iliopepesuka mwishoni mwa wiki:stuttgart iliozabwa mabao 2:1 na Schalke.

Hatahivyo, Stuttgart ,ikiwa katika kundi G, inaumana kesho na Sevilla na kwavile inacheza nyumbani Daimler Stadium, mashabiki wake wanatazamia Stuttgart itafuta madhambi iliofanya mwishoni mwa wiki ilipoiachia schalke kutamba. Sevilla ya Spian ndio inayoongoza kundi hili G, linajumuisha pia Glasgow rangers, inapambana na Unirea Urziceni.

Kesho,mabingwa wa zamani wa Ulaya Bayern Munich watakuwa Ufaransa kwa miadi na Girondis Bordeeaux.wakati Munich ilitamba mwishoni mwa wiki ilipoilaza Freiburg katika bundesliga, Bordeaux iliteleza katika Ligi ya Ufaransa.

Mabingwa wa Ujerumani ,Wolfsburg wamejiwinda nyumbani kuwakaribisha waturuki Besiktas Istanbul hapo Jumatano. Baada ya kulazwa 2:1 na Manu huko Uingereza, Wolfsburg,wanahitaji ushindi wao wa kwanza katika Champions League .

Mwishoe, kura imepigwa hivi punde kuamua kanda ya ulaya ni timu gani 4 zitatoroka na tiketi za mwisho za Kombe lijalo la dunia huko Afrika Kusini:Ureno inayotamba na Cristiano Ronaldo na yenye hamu kuu kwenda Afrika kusini,inabidi kucheza na Bosnia.Ukraine itapambana na Ugiriki wakati Russia itabidi kukata tiketi yake kupitia Slovenia.

Mwandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Abdul-Rahman