1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfowitz mashakani

Josephat Charo13 Aprili 2007

Rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, anakabiliwa na shikizo kubwa katika maisha yake ya kisiasa hii leo baada ya bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo kufichua ushahidi uliovunja makali ushahidi wake kuhusu kashfa ya upendeleo inayomhusu mpenzi wake, Shaha Riza. Bodi ya magava imeahirisha mkutano uliotarajiwa kuzungumzia kuongezewa mshahara mkubwa Shah Riza uliozusha manung´uniko miongoni mwa wafanyakazi wa benki ya dunia.

https://p.dw.com/p/CHGK
Rais wa benki ya dunia Paul Wolfowitz
Rais wa benki ya dunia Paul WolfowitzPicha: picture-alliance/dpa

Huku miito ya kumtaka rais wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz, ajiuzulu ikizidi kuongezeka, wakurugenzi watendaji wa bodi ya benki hiyo wametoa taarifa ambayo imemuweka mahali pabaya kiongozi huyo. Bodi hiyo imaehirisha mkutano wake wa leo kuzungumzia swala hilo lakini ikasema itafanya haraka kuamua itakavyoishughulikia kashfa hiyo.

Baada ya mkutano wa dharura jana ulioendelea mpaka usiku, bodi hiyo ilitoa maelezo ya kina kuhusu matokeo ya uchuhguzi wao kuhusiana na mzozo unaomhusu Wolfowitz na mpenzi wake mzaliwa wa Libya, Shaha Riza. Kurasa zaidi ya 100 zilizotolewa pamoja na taarifa ya bodi hiyo, zimedhihirisha kwamba Wolfowitz aliamuru Shaha Riza aongezewe mshahara kufikia karibu dola laki mbili wakati alipohamishwa kufanya kazi katika wizara ya ndani ya Marekani kwa niaba ya benki ya dunia wakati alipochukua hatamu za uongozi katika benki hiyo mnamo mwezi Juni mwaka wa 2005.

Wolfowitz anasema alifuata ushauri wa kamati ya maadili ya benki ya dunia. ´Nilifanya juhudi kufanya nilichofahamu katika ushauri wa kamati ya maadili ya benki ya dunia. Na nilifanya hivyo ili kubeba dhamana kukamilisha jambo nililoamini linaweza kuiharibu taasisi hii.´

Ushahidi mpya unajumulisha kumbukumbu iliyoandikwa na Wolfowitz kwa idara ya huduma za wafanyakazi ya benki ya dunia mnamo mwezi Agosti mwaka wa 2005 ambapo aliiamuru idara hiyo imuongezee mshahara mpenzi wake Shaha Riza.

Taarifa ya bodi ya benki ya dunia imesema wakurugenzi watafanya haraka kufikia uamuzi hivi karibuni kuhusu hatua wanazoweza kuchukua dhidi ya Wolfowitz huku wakizingatia athari katika uongozi wa benki hiyo. Bwana Wolfowitz alisema jana kwamba atakubali mapendekezo yatakayotolewa na magavana wa bodi hiyo huku akijiandaa kwa mkutano wa kila mwaka wa benki ya dunia wikendi hii ambao ajenda yake inatarajiwa kugubikwa na kashfa hiyo.

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Washington, Wolfowitz alijutia kitendo alichokifanya. ´Afadhali kama ningeamini hisia zangu za awali na kujitenga na mazungumzo ya kumuongezea mshahara mkubwa Shaha Riza. Nilifanya makosa ambayo nayajutia na naomba msamaha.

Lakini matamshi yake hayakutosha kwa chama cha wafanyakazi wa benki ya dunia kikisema Wolfowitz ameharibu imani ya wafanyakazi na anatakiwa ajiheshimu na ajiuzulu. Katika toleo lake la leo gazeti la Finacial Times pia limemtaka Wolfowitz ang´atuke aidha kwa hiari au atimuliwe na bodi ya magavana.

Wolfowitz anakabiliwa pia na shinikizo kutoka kwa wafanyakazi wenzake kwa mfumo wake wa uongozi kufuatia malumbano kadhaa na bodi ya benki ya dunia kwa kuwapa kazi washirika wake wa chama cha Republican katika benki hiyo. Wolfowitz amesisitiza kwamba anapenda kuendelea na kazi yake ili kulifikia lengo la kupunguza umaskini duniani kote.