1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfgang Schaueble spika mpya Bundestag

Sekione Kitojo
24 Oktoba 2017

Waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble amechaguliwa kuwa spika mpya wa bunge la Shirikisho Bundestag, ambapo atajaribu kudhibiti nidhamu kwa wabunge wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD.

https://p.dw.com/p/2mQh1
USA G20 IMF Pressekonferenz Wolfgang Schäuble
Picha: Imago/photothek/T. Köhler

Wakati  huo  huo  chama  cha  mrengo  mkali  wa  kulia  cha AfD kimeapa kwamba  enzi  mpya  imewadia  nchini  Ujerumani  wakati kikishiriki kwa  mara  ya  kwanza  kikao cha bunge jipya , ambapo kimeweza kuonesha  ubavu  wake.

Sekione  Kitojo  na  taarifa  zaidi.

Wolfgang  Schaeuble  alichaguliwa  kuwa  spika  wa  bunge  kwa kupata  kura 501 kati  ya  kura  705 zilizopigwa  na  wabunge wenzake  kwa  ajili  ya  wadhifa  huo  wa  bunge la  taifa , Bundestag.

Deutschland 1. Sitzung im neuen Bundestag
Wolfgang Schaueble spika mpya wa bunge la Ujerumani BundestagPicha: Reuters/H. Hanschke

 "Bwana Mwenyekiti nimekubali matokeo ya uchaguzi."

Wolfgangn Schäuble ametilia mkazo umuhimu wa watu kuheshimiana bungeni,akisemam unabidi uwe mfano kwa jamii. Mnamo miezi iliyopita kauli za kuvunjiana hishma na kudharauliana zimekuwa zikisikika. Kauli kama hizo hazina nafsi  katika  bunge atakaloliongoza  amesema Schaeuble.

Chama  cha  Alternative  for Germany , chama  mbadala  kwa Ujerumani , AfD , ambacho  kilifanikiwa  kuingia  bungeni  kwa  mara ya  kwanza katika  uchaguzi  wa  mwezi  uliopita, mara  moja kilionesha  kwamba  kitaleta  changamoto kubwa  bungeni  hapo baadaye.

Deutschland 1. Sitzung im neuen Bundestag
Spika mpya wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaueble akipongezwa na kansela Angela Merkel (kushoto)Picha: Reuters/F. Bensch

Hoja ya  kwanza bungeni

Kikionesha  kwamba  kutakuwa  na  mivutano  zaidi  bungeni  katika miaka  minne  ijayo  chama  cha  AfD  kilikuwa  cha  kwanza kuwasilisha  hoja  bungeni  kupinga  mabadiliko  katika  sheria  za bunge  ambazo  zinazuwia  mmoja  kati  ya  wabunge  wake  kutoa hotuba ya  ufunguzi  katika  bunge  hilo.

Wakati  hoja  hiyo ilishindwa mara  moja  na  wabunge  wengine  wote, mkuu  wa kundi  la wabunge  wa  chama  cha  AfD bungeni Bernd Baumann alifananisha  hali  hiyo na  hatua  ya  Hermann Goering wakati  wa enzi  za  Wanazi mwaka  1933  alipomzuwia  kiongozi  wa  kikomunist Clara Zetkin  kutoa  hotuba  ya  ufunguzi katika  kikao  cha  bunge.

Matamshi  hayo  yalipokelewa  kwa  mshangao  mkubwa  wa wabunge  na  kushutumiwa  na  mbunge  wa chama  cha  Free Democrats FDP Marco Bueschmann  kuwa, hayakuwa  na  mashiko.

Lakini  mashambuliaji  hayo  yanaonekana  kama  mwanzo  wa mivutano  mikali  katika  vikao  vijavyo, wakati wabunge  waandamizi katika  chama  cha  AfD wamekuwa  mara  kwa  mara  wakivunja utaratibu  kwa  kutoa  madai  ya  uasili wa Ujerumani  na  kutoa changamoto  kwa  utamaduni  wa  Ujerumani  wa  kujihisi  na makosa kuhusiana  na  vita  vikuu  vya  pili  vya  dunia  pamoja  na mauaji  ya  wayahudi  ya  Holocaust.

Bundestagssitzung Bundestag Berlin
Mbunge wa chama cha AfD Bernd BaumannPicha: Reuters/H.Hanschke

Baumann amesema , Bunge  la  zamani  limemaliza  muda  wake. wananchi  wameamua , enzi  mpya  inaanza  sasa." Kuanzia  sasa , masuala  yatajadiliwa  upya, sio mbinu  zenu na  ujanja  mnaofanya bungeni lakini  masuala  kama  sarafu  ya  euro, deni  kubwa, idadi kubwa  wa  wahamiaji, mipaka iliyo  wazi  na  uhalifu  mkubwa  katika mitaa  ya  miji  yetu, ameongeza  Baumann.

Mpambano  mwingine  unafukuta  leo  wakati  wabunge watakapochagua  makamu  wa  spika. Kila  chama  kina  haki  ya kumteua makamu  wake  katika  bunge, lakini  yeyote  awaye anapaswa  kupigiwa  kura  bungeni.

Mwandishi:   Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri:   Mohammed  Abdul Rahman