1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la Wakimbizi Magazetini

21 Oktoba 2016

Nchi za Umoja wa Ulaya na wimbi la wakimbizi kutoka Afrika, Ethiopia na visa vya ukandamizaji na hukumu ya Korti ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague,ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2RWEa
Frankreich | Das Flüchtlingslager Calais kurz vor der Schließung - erste Flüchtlinge verlassen den Jungle
Picha: REUTERS/ P. Rossignol

 

Tuanze lakini na mada iliyohanikiza nchini Ujerumani na katika nchi za Umoja wa Ulaya kwa jumla: mada kuhusu wakimbizi wanaotokea Afrika. "Mwisho wa desturi za kuwakaribisha watu" au Umoja wa Ulaya unataka kuwarejesha wakimbizi zaidi wa Kiafrika makwao" ndio vichwa vya maneno vya ripoti mbili za gazeti la mjini Berlin, die Tageszeitung au taz kwa ufupi. Gazeti hilo linazungumzia kwanza kuhusu uamuzi uliopitishwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ulioitishwa Alkhamisi na Ijumaa iliyopita mjini Brussels, ambapo viongozi walihimiza ifungwe kabisa njia kuu inayotumiwa ya wakimbizi wanaoyatia hatarini maisha yao katika Bahari ya Kati ili kuweza kuingia Italia. Njia hiyo hutumiwa zaidi na wakimbizi kutoka Afrika.

Na ili kuzuwia wimbi la wakimbizi hao, nchi za Umoja wa Ulaya, linaendelea kuandika gazeti la die Tageszeitung, zinapanga kupanua makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Jordan na Lebanon, hadi katika nchi za Afrika, zikihusishwa Niger, Nigeria, Senegal, Mali na Ethiopia. Na kwa mujibu wa gazeti hilo la mjini Berlin, serikali kuu ya Ujerumani inataka Misri na Tunisia pia zijumuishwe. Uamuzi wa mwisho unategemewa pale viongozi wa Umoja wa Ulaya watakapokutana mwezi wa Desemba mjini Brussels, linamaliza kuandika gazeti la die Tageszeitung lililokumbusha ziara iliyofanywa mwezi huu na Kansela Angela Merkel katika nchi tatu za Afrika: Mali, Niger na Ethiopia - ziara iliyofuatiwa siku ya pili yake na kukaribishwa mjini Berlin, Rais Idriss Deby wa Chad na baadaye mwenzake wa Nigeria, Muhammadu Bouhari.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung limezungumzia zaidi misaada zaidi ya fedha inayopangwa kutolewa kuchochoea maendeleo ya kiuchumi na kusema misaada hiyo haitozuwia wimbi la wakimbizi kutoka Afrika. Süddeutsche linakumbusha bara la Afrika ni tajiri na kwa miaka kadhaa sasa wenye vipaji kutoka Afrika wamekuwa wakipatiwa mafunzo katika nchi za Ulaya. Zaidi ya hayo, watu wote mpaka wa vijijini wanaweza kujipatia siku hizi maarifa kupitia mtandao. Ikiwa njia zote hizo zitatumiwa, nyengine zitafuata. Tukishindwa kufuata mpangilio huo, tutakuwa tunakwenda kinyume na msingi wenyewe hasa wa kusaidia. Na hilo hasa ndilo linalofanyika tangu zamani - linamaliza kuandika gazeti la mjini Munich la Süddeutsche.

Kukandamizwa haki za rais nchini Ethiopia

Ethiopia pia imegonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika: "Ukandamizaji usiokwisha. Badala ya kutekeleza ahadi za kuacha milango wazi, serikali ya Ethiopia inaendelea kuuwekea vizuwizi uhuru." Frankfurter Allgemeine linazungumzia sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa mapema mwezi huu wa Oktoba, ambayo serikali ya Ethiopia imeitumia kama kisingizio cha kukandamiza uhuru wa watu kwenda wakutakako na pia kutoa maoni yao.

Kwa namna hiyo, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine, serikali ya Ethiopia imetaka kuwafumba midomo wale wanaoandamana kudai demokrasia zaidi katika majimbo ya Oromia na Amhara. Waethiopia wamepigwa marufuku pia kutumia mitandao ya kijamii "eti wasije wakawasiliana na watu walioko nje". Wanaotajwa hapo ni Waethiopia wanaoishi Ulaya na Marekani ambao daima wamekuwa wakikosoa visa vya kikatili vya vikosi vya usalama. Frankfurter Allgemeine limekumbusha haki za mtu kwenda akutakako na haki ya mtu kutoa maoni yake zinadhaminiwa na katiba ya nchi hiyo.

 ICC yawahukumu  Bemba na Mawakili wake

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inachambuliwa na gazeti la die Tageszeitung linalosema kwa mara ya kwanza Korti ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague imewahukumu mawakili na wanaemtetea. Makamo wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jean-Pierre Bemba, na mawakili wake wanne wametiwa hatiani kwa makosa ya kuwahonga mashahidi ili waseme uwongo na kumtoa hatiani.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSEER/ALL/Presse

Mhariri: Mohammed Khelef