1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaanzisha kitengo cha kupambana na Zika

2 Februari 2016

Shirika la Afya Duniani-WHO, limeanzisha kitengo cha kimataifa kukabiliana na virusi vya Zika, huku likielezea hofu yake kuhusu ugonjwa huo kwamba unaweza ukaenea hadi barani Afrika na Asia.

https://p.dw.com/p/1HoBz
Aedes aegypti mosquito - Zika Virus
Picha: Reuters/J. Saldarriaga

Mtaalamu wa Shirika la Afya Duniani-WHO, Dokta Anthony Costello amesema leo kuwa shirika hilo limeanzisha kitengo maalum ili kukabiliana na virusi vya Zika, baada ya jana shirika hilo kutangaza kwamba virusi vya Zika vinavyosababishwa na mbu, kuwa dharura ya kiafya duniani na wanautaja ugonjwa huo kuwa chanzo cha watoto kuzaliwa na ulemavu na hasa kuzaliwa na kichwa kidogo pamoja na ubongo ulioathirika katika eneo la Amerika ya Kusini, ingawa bado hakuna ushahidi wa kutosha kuhusu hilo.

''Asubuhi hii tumeunda kitengo maalum kitakachowakutanisha pamoja watu wote katika makao makuu ya WHO katika ukanda huo, ili kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutumia mafunzo tuliyoyapata kutokana na mzozo wa Ebola,'' alisema Dokta Costello.

Shirika hilo liko katika shinikizo la kukabiliana haraka na virusi vya Zika, baada ya kukiri kuwa iliushughulikia taratibu ugonjwa wa Ebola uliolikumba eneo la Afrika Magharibi.

Kitengo hicho kujifunza kutokana na Ebola

Costello ambaye ni daktari bingwa wa watoto na mtaalamu wa matatizo ya watoto wenye vichwa vidogo, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba kitengo hicho kipya kilichoundwa kitakuwa na lengo la kujifunza kutokana na namna walivyoushughulikia mzozo wa Ebola, ili kusaidia haraka kuutafutia ufumbuzi ugonjwa wa Zika na kasoro zinazowapata watoto ambazo zinaaminika kusababishwa na virusi vya Zika.

Amesisitiza kuhusu haja ya kuchukuliwa hatua za haraka akisema hakuna uhakika kwamba virusi vya Zika vitabakia tu kwenye nchi 25 za Amerika ambazo tayari zimetangaza kuwa na visa vya ugonjwa huo. Costello amesema wana hofu kuwa virusi hivyo vinaweza vikasambaa kwenye maeneo mengine ya dunia ambako watu wake wanaweza wasiwe na kinga na wanajua kwamba aina ya mbu wanaoeneza ugonjwa wa Zika, wanapatikana sana kwenye maeneo mengi ya Afrika, sehemu za kusini mwa Ulaya na maeneo mengi ya Asia, hasa kusini mwa Asia.

Mtaalam akiwa maabara akiwachunguza mbu wanaoeneza virusi vya Zika
Mtaalam akiwa maabara akiwachunguza mbu wanaoeneza virusi vya ZikaPicha: Reuters/P. Whitaker

Wakati huo huo, shirika lisilo la kiserikali la Uholanzi limeanzisha juhudi za kimataifa za kuwapatia wanawake wajawazito wanaougua ugonjwa wa Zika, vidonge vinavyosababisha mimba kutoka, kwa lengo la kuzuia uharaka wowote wa wanawake hao kutoa mimba katika njia zisizo salama.

Mkurugenzi wa shirika hilo la wanawake kwenye mtandao, Rebecca Gomperts amesema wana hofu kuwa virusi hivyo vinaweza kuongeza utoaji wa mimba usio salama na kwamba wao wanajali sana afya na maisha ya wanawake, hivyo wanataka kuhakikisha wanawake wanatoa mimba katika mazingira mazuri ya matibabu.

Virusi vya Zika vinaambukizwa na mbu aina ya Aedes Aegypti, ambaye pia anaeneza homa ya Dengue na Chikungunya na aligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka 1947.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu