1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Westerwelle ataka Assad afikishwe mahakamani

Majeshi ya serikali ya Syria yameendelea kuwashambulia waasi kwa mizinga katika mji wa Aleppo,kaskazini mwa Syria.Na Waziri Westerwelle ataka Assad afikishwe mahakamani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema anataka Rais Bashar al-Assad wa Syria afikishwe mbele ya Mahakama ya Kimataifa kujibu mashtaka ya kutenda uhalifu wa kivita. Waziri Westerwelle amesema jambo muhimu kwa sasa ni kuyakomesha mauaji nchini Syria na kuhakikisha mustakabal wa amani.Hata hivyo waziri huyo wa Ujerumani kwa mara nyingine amepinga ujiingizaji wa kijeshi nchini Syria kutoka nje.

Wakati huo huo Marekani na Uturuki zinatafakari njia zote za kuwasaidia waasi wanaopigana ili kuuangusha utawala wa Bashar al-Assad. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton aliye ziarani nchini Uturuki, amesema njia hizo ni pamoja na kuzipiga marufuku ndege za majeshi ya serikali ya Syria kuruka katika maeneo fulani ya anga.

Baada ya mazungumzo na waziri mwenzake wa Uturuki Ahmet Davutoglu, Waziri Clinton aliwaambia waandishi wa habari mjini Istanbul, kwamba Marekani na Uturuki zinahitaji kupanga mikakati ya jinsi ya kuwasaidia waasi ili kukomesha mauaji nchini Syria.

Waziri Clinton amesema idara za usalama za Marekani na Uturuki zina dhima muhimu ya kutimiza na kwa hivyo nchi hizo zitaunda kamati za kazi zitakazoitekeleza dhima hiyo.Waziri huyo wa Marekani amesema amekubaliana na Waziri mwenzake wa Uturuki juu ya suala la kuzizuia ndege za jeshi la Syria kuruka katika maeneo fulani ya anga.Lakini hakusema ni lini hatua hiyo inaweza kuchukuliwa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/rtr/afp

Mhariri:Amina Abubakar

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com