1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wengi wajitokeza kupiga kura Kenya

27 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CguK

NAIROBI. Maelfu ya wananchi wa Kenya leo wamejitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Rais Mwai Kibaki anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha ODM, Raila Odinga ambaye kwa mujibu wa kura za maoni alikuwa mbele ya kibaki kwa asilimia chache kabla ya kura za leo.

Mgombe mwengine kati ya wanane wa Urais ni waziri wa zamani wa mambo ya nje Kalonzo Musyoka wa chama cha ODM-KENYA.

Mapema Raila Odinga alishindwa kupinga kura katika muda aliyopanga baada ya jina lake kukosekana katika daftari la wapiga kura.

Hata hivyo baadaye Raila alipiga kura yake ambapo alisema kuwa chama chake kitapata ushindi mkubwa.

Kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya Alexander Graf Lambsdorff ameitaka tume ya uchaguzi kuongeza muda wa saa mbili zaidi kupiga kura katika kituo hicho kutokana na wingi wa watu.

Kwa upande wake Rais Mwai Kibaki akizungumza baada ya kupiga kura yake kwenye mji wa Nyeri alisema kuwa ana uhakika na ushindi.

Lakini alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo atashindwa na Raila, atayakubali matokeo,Rais Kibaki aliwajibu waandishi hao kuwa waache maswali yao ya kipuuzi.

Takriban watu millioni 14 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo, ambao umegubikwa na wasi wasi wa wizi wa kura na ghasia.

Katika eneo la Kisumu Polisi watatu waliuawa, baada ya wafuasi wa upande wa upinzani kuwatuhumu kuwa walikuwa wamebeba karatasi za kura za wizi.

Zaidi ya wa waangalizi elfu 15 wa ndani na nje wanaufatilia uchaguzi huo.