1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani ziarani Afghanistan

Oumilkher Hamidou10 Machi 2009

Mwito wa kuzungumza na wataliban wa nadharia za wastani wakataliwa na msemaji wa Mullah Omar

https://p.dw.com/p/H9BL
Waziri wa ulinzi Franz Josef JungPicha: picture-alliance/ dpa


Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,Franz Josef Jung,amewatolea mwito hii leo wataliban wanaofuata itikadi kali waweke chini silaha na kusaka ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo


Akiwazuru wanajeshi wa Ujerumani katika mji wa kaskazini wa Feysabad hii leo,waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,Franz Josef Jung amewasihi waasi "waachane na matumizi ya nguvu na kufuata njia ya amani."


Mwito wa kushiriki katika meza ya mazungumzo umekataliwa kwa mara nyengine tena na msemaji wa mkuu wa wataliban Mullah Omar,jambo linalodhihirisha kwamba Mullah Omar anapendelea zaidi kuendeleza matumizi ya nguvu,na msimamo mkali .


Msemaji wa wataliban Sabihullah Mudschahed ameuambia mtandao wa "Spiegel Online","mwito wa kushirikishwa waasi katika meza ya mazungumzo",hauna maana yoyote."Hakuna mtaliban wa nadharia ya wastani nchini Afghanistan,kuna vugu vugu la wataliban tuu na hatuko tayari kuzungumza.Wapiganaji wetu na makamanda wetu wanatii amri ya Mullah Omar tuu na hawatozungumza na mtu.Mazungumzo pamoja na serikali ya mjini Kaboul yatawezekana tuu ikiwa masharti ya wataliban ya kuhamishwa wanajeshi wote wa kigeni yatatekelezwa."Amesema hayo msemaji wa wataliban aliyekanusha ripoti kwamba wataliban wanaweza kukubali shauri la kuweka chini silaha."


Akituwa kwa muda nchini Uzbekistan jana usiku,waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Franz Josef Jung alisisitiza mazungumzo yafanyike tuu pamoja na makundi ya wataliban wasiotumia nguvu."


Amekumbusha mtihani uliowafika waengereza katika juhudi zao za kutaka kuzungumza na wataliban wa nadharia za wastani kusini mwa Afghanistan.


Waziri wa ulinzi Franz Josef Jung alikitembelea pia kituo cha mafunzo ya Polisi huko Masar-i Sharif na kusifu ufanisi uliopatikana hadi sasa.Waziri Jung aliwatembelea kwanza wanajeshi huko Mazar i Sharif kabla ya kwenda Faysabad kuwazuru wawakilishi wa  Ujerumani wanaoshiriki katika juhudi za kuijenga upya Afghanistan.


Ujerumani imetuma wanajeshi 3800 nchini Afghanistan kutumikia kikosi cha kimataifa cha ISAF.Ujerumani ni nchi yatatu baada ya Marekani na Uengereza kutuma wanajeshi wengi nchini Afghanistan.