1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Israel ziarani Washington

Oumilkher Hamidou1 Juni 2009

Ehud Barack amedhamiria kusawazisha mvutano wa pande mbili

https://p.dw.com/p/I1Qb
Waziri wa ulinzi Ehud Olmert (kulia)Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak anatazamiwa kuitembelea Marekani leo. Atajaribu wakati wa ziara hiyo kupunguza mwanya unaoitenganisha nchi yake na mshirika wake mkubwa,kuhusu utaratibu wa amani ya mashariki ya kati.

Barack anataraajiwa kutumia wakati mrefu wa ziara yake kupunguza mivutano,ingawa mazungumzo yalipangwa hapo awali kulenga mafungamano ya pande mbili ya ulinzi na juhudi zinazoongozwa na Marekani za kuzuwia kiu cha Iran cha kujipatia silaha za kinuklea.

Katika ziara hiyo ya siku tatu,waziri wa ulinzi wa Israel anatazamiwa kukutana na makamo wa rais Joe Biden,waziri wa ulinzi Robert Gates,Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa James Jones na mjumbe maalum wa rais Barack Obama katika eneo la Mashariki ya kati George Mitchell.

Waziri huyo wa ulinzi wa Israel anatazamiwa pia kuzungumzia biashara ya silaha za Marekani kwa Israel,ikiwa ni pamoja na maombi ya kununua madege 75 ya kijeshi ya chama F-35- na zana nyengine za kimambo leo za kiijeshi.

Ziara ya waziri wa ulinzi Ehud Barack inafanyika wiki mbili baada ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu kukutana kwa mara ya kwanza kwa mazungumzo pamoja na rais Barack Obama mjini Washington,ziara iliyobainisha hitilafu za kina za maoni kuhusu njia inayostahiki kufuatwa kuelekea amani ya Mashariki ya kati.

Benjamin Netanjahu spricht auf einer Wahlkampfveranstaltung in Tel Aviv
Waziri mkuu wa Israel NetanyahuPicha: AP

Waziri mkuu huyo shupavu amesababisha lawama za walaimwengu kwa kukataa kwake kuunga mkono fikra ya kuundwa dola ya Palastina-kiini cha juhudi za amani kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Mivutano imezidi makali baada ya Israel kupuuza nasaha za mara kwa mara ya Marekani za kusitisha ujenzi wa makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za waarabu zinazokaliwa katika ukingo wa magharibi-zinazoangaliwa kama sehemu kubwa ya dola la sikuu za mbele la wapalastina.

Ehud Barack,aliyewahi kua waziri mkuu na kiongozi wa chama cha mrengo wa kati ya kushoto-Labour,amedhamiria kutumia mafungamano aliyonayo kuepusha mgogoro kati ya washington na serikali ya mrengo wa kulia ya Benjamin Netanyahu.

Haijulikani lakini kama Ehud Barack atafanikiwa kupunguza makali ya mvutano kwakua yeye mwenyewe ameshasema Israel inastahiki kuendelea kujenga majumba ya wahamiaji wa kiyahudi.

"Yadhihirisha kana kwamba waziri mkuu amefafanua msimamo na mahitaji ya Israel kwa utawala wa Marekani.Mdahalo utahitaji muda na mivutano haitakosekana." alisema hayo kiongozi huyo wa Labour mbele ya waandishi wa habari.

Inatarajiwa Ehud Barack huenda akapendekeza kubomolewa katika kipindi kifupi kijacho,makaazi ya wahamiaji yaliyojengwa kinyume na sheria katika vitongoji vya ukingo wa magharibi,ikiwa Marekani itaikubalia Israel iendelee kujenga ili kukidhi "muongezeko wa kimaumbile" wa walowezi wa kiyahudi.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel amelalamika na kuhoji utawala wa rais Barack Obama wa Marekani,uliopania kuendeleza mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati "unaitaka Israel ipitishe hatua ambazo ni sawa na kujitolea mhanga,wakati wapalastina hawaambiwui chochote".

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman