Waziri Steinmeier wa Ujerumani atembelea gavana Schwarzenegger wa California | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Steinmeier wa Ujerumani atembelea gavana Schwarzenegger wa California

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Bw. Frank-Walter Steinmeier, aliye ziarani nchini Marekani ametoa mwito kwa nchi hiyo kubwa kushiriki katika juhudi za pamoja kulinda mazingira na kuzuia ongezeko zaidi la ujoto duniani. Steinmeier leo hii anakutana na mwanasiasa mwingine wa Marekani ambaye analipigia debe suala la ulinzi wa mazingira, yaani gavana wa jimbo la California.

Kalifornien inayapigia debe matumizi nishati endelevu

Kalifornien inayapigia debe matumizi nishati endelevu

Nchini Marekani, jimbo la California linachukua nafasi ya kwanza katika kuongoza nchi hiyo kuelekea sera za ulinzi wa Mazingira. Upande wa sheria, California imeweka kiwango cha chini kabisa cha utoaji wa gesi chafu na imejiwekea malengo makubwa kupunguza utoaji wa hewa chafu ya Carbondioxide inayoharibu hali ya hewa. Kulingana na malengo haya, utoaji wa gesi chafu unatakiwa kupunguzwa kwa asilimia 25 hadi mwaka 2020. Vilevile, katika muda wa miaka mitatu, California inataka asilimia 20 ya umeme utengenezwe kwa kutumia nishati endelevu. Magari pia yamewekewa sheria kali juu ya moshi yanayotoa ambao unatakiwa upunguzwe kwa asilimia 30 katika muda wa miaka kumi.

Gavana wa jimbo hili, Bw. Arnold Schwarzenegger ambaye aliwahi kuwa mchezaji maarufu wa filamu, siku hizi ni kama msemaji wa wale nchini Marekani ambao wanayajali mazingira. Tena anaikosoa vikali sera ya hali ya hewa ya rais Bush, ingawa yeye ni wa kutoka chama chake cha Republican: “Katika vita dhidi ya ongezeko la joto duniani, Marekani haijafikia pale inapotakiwa kuwepo. Hatua funali zinachukuliwa, lakini si kwa kasi ipasavyo. Tena hatua hizo hazitoshi. Ombi langu ni kwamba serikali ibebe dhamama kubwa zaidi.”

Kabla ya kukutana na gavana Schwarzenegger, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alitoa mwito kwa Marekani kushirikiana na Ujerumani kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa. Alipohudhuria mkutano wa makampuni ya Kijerumani jimboni California, Steinmeier alisema pindi nchi hizo mbili zitakapochukua hatua kwa pamoja kuna nafasi ya kuishawishi dunia nzima kwamba ni lazima kulinda mazingira na kuhifadhi hali ya hewa. Kabla ya kufika Marekani, Steinmeier alitembelea eneo la Kaskazini mwa bara la Ulaya ambapo aliwahi kuona vile barafu inazidi kuyeyuka. Jimboni California, waziri Steinmeier alitaka kuangalia teknolojia za kisasa zinazotumia nishati ndogo au aina nyingine ya nishati. Katika kuendeleza teknolojia Marekani na Ujerumani zinapaswa kushirikiana, Steinmeier alisema.

Inatarajiwa kuwa atakuwa na mazungumzo mazuri na gavana Schwarzenegger, kwani huyu anaimba wimbo huo huo: “Licha ya California ni ndogo ikilinganishwa na ulimwengu, tuna uwezo mkubwa ambao uko sawa na ule wa mabara mazima. Ninataka kutumia uwezo wetu kuyashawishi mataifa mengine yashirikiane nasi kulinda mazingira. Katika vita dhidi ya ongezeko la ujoto duniani tunaweza kushinda tu ikiwa tunashirikiana.”

Hata hivyo, Schwarzenegger anakabiliwa na upinzani kutoka sekta ya uchumi. Makampuni yanalaumi kuwa urasimu mwingi unawazuia kutumia nishati endelevu.

Katika mazungumzo yao leo, waziri Steinmeier na gavana Schwarzenegger watazungumzia pia uwezekano wa kushirikiana katika biashara ya ruhusa za utoaji gesi. Barani Ulaya kuna biashara ya leseni za kutoa gesi chafu. Nchini Marekani mfumo kama huo pia unaandaliwa na majimbo kadhaa.

 • Tarehe 30.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8l
 • Tarehe 30.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8l

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com