1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan kurejea kutoka uhamishoni

25 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSqW

Rais wa Pakistan Jemadari Pervez Musharraf huenda akakabiliwa na changamoto kali,baada ya waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif,kuamua kurejea nyumbani kutoka uhamishoni nchini Saudi Arabia. Sharif,aliepinduliwa na Musharraf miaka minane iliyopita,anatazamiwa kuwasili hii leo mjini Lahore,mashariki mwa Pakistan huku nchi ikiyumba kutokana na mashambulizi ya kujitolea muhanga. Siku ya Jumamosi,hadi watu 35 waliuawa katika mashambulizi mawili yaliyotokea takriban wakati mmoja katika mji wa Rawalpindi.

Wapakistani wengi wanalalamika kuwa hali ya hatari iliyotangazwa na Rais Musharraf mapema mwezi huu,imewazima wakosoaji wa Musharraf lakini haikutuliza machafuko ya wanamgambo.Kurejea kwa Nawaz Sharif huenda kukabadili hali ya kisiasa nchini Pakistan,ambako wapinzani wametishia kugomea uchaguzi unaotazamiwa kufanywa Januari 8 mwakani.