1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Israel na Mahmud Abbas

V.Clemens20 Novemba 2007

Waziri mkuu wa Israel ghafula leo amefunga safari ya Sham El Sheikh kuonana na rais Hosni Mubarak wa Misri

https://p.dw.com/p/CLTY
Abbas na OlmertPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert, anatazamiwa nchini Misri leo kwa mkutano nadra na rais Hosni Mubarak na kabla ya mkutano wa amani ulioandaliwa na Marekani huko Annapolis,baadae mwezi huu.

Serikali ya Israel, imeidhinisha jana kuachwa huru kwa wafungwa 441 wa kipalestina-wengi wao ni wanachama wa chama cha FATAH.Mamlaka ya ndani ya wapalestina, haikuridhishwa na idadi ndogo kama hiyo.Kiasi cha wapalestina 10.000 wamo gerezani nchini Israel.

Mazungumzo kati ya waziri mkuu Olmert na rais Hosni Mubarak huko Sharm el-Sheikh, yanafanyika baada ya Olmert na rais Mahmud Abbas wa Palestina kushindwa kuafikiana hapo jana juu ya tamshi la pamoja ambalo lingejenga msingi wa kuamua juu ya mazungumzo ya hatima ya mwisho ya ardhi za wapalestina.

Marekani imeutisha mkutano huo wa Annapolis, kukwamua ule mpango wa njia ya amani “Road map” ulionasa tangu miaka 7 sasa.Matumaini ya maafikiano tayari yamefifia kutokana na kutoridhiana huko kwa pande hizi mbili.

Pande zote mbili zimepiga hatua katika maswali fulani ya kutolewa taarifa hiyo ya pamoja ,lakini hakuna bado maafikiano juu ya maswali mengine.”Afisa wa hadhi ya juu wa Israel aliarifu.Akungama hayo, waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert alithibitisha:

“Ukweli ni kuwa zipo tofauti.Na hii hatufichi.Tunapaswa kuafikiana juu ya baadhi ya maswali.Tunatumai kukubaliana juu ya utaratibu wa kufuatwa kwa maandalio ya mkutano wa Annapolis.M ajadiliano hasa yatafanyika baada ya kikao cha Annapolis.”

Mjumbe mkuu wa wapalestina Saeb Erakat aliwaambia maripota huko Ramallah,Ukingo wa magharibi na ninamnukulu,

“kuna tofauti ,mkutano ulikua mgumu,tofauti zimesalia na pande mbili zinakutana tena leo usiku.”

Wapalestina kwa upande wao inavuma kwamba watawakilisha masilahi yao barabara na hawataregeza kamba na hii imefahamika kandoni mwa duru za waziri mkuu Olmert.Msimamo huo mkali wa wapalestina utachukua sura hii:

Endapo haitawezekana kumfanya waziri mkuu Olmert kuafuikiana tangazo la pamoja kwa mkutano wa mashariki ya kati huko Annapolis,upande wa Palestina utatoa tangazo lake binafsi.

Kwa jicho hili kuachwa huru kwa wafungwa 441 kulikoidhinishwa na serikali ya Israel hapo jana kumeelezwa na waziri wa Palestina anaehusika na maswali ya wafungwa Al Ajrami hakuridhishi kabisa.

“Hii ni hatua ndogo tu iliochukuliwa na Israel,kwani azma yetu ni kuachwa huru kwa maalfu ya wafungwa wa kipalestina.Israel bila ya shida yoyote, yamudu kuwafungua zaidi ya wapalestina 7.000 hata chini ya vipimo vya Israel yenyewe.”

Israel jana iliahidi kukomesha ujenzi wa maskani zaidi za wayahudi katika ukingo wa magharibi na msemaji wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina, Riyad al-Maliki aliukaribisha uamuzi huo.