1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu mpya wa Mali aapa kuikomboa kaskazini

12 Desemba 2012

Rais wa Mali Dioncounda Traore amemteua Diango Sissoko kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo, baada ya kujiuzulu kwa Cheick Modibo Diarra. Sissoko amesema kipaumbele ni kuikomboa sehemu ya kaskazini ya nchi.

https://p.dw.com/p/170GQ
Waziri mpya wa Mali aapa kuikomboa kaskazini
Waziri mpya wa Mali aapa kuikomboa kaskaziniPicha: Reuters

Diango Sissoko ameteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa Mali, saa 24 tu baada ya mtangulizi wake Cheick Modibo Diarra kujiuzulu kutokana na tofauti za kisiasa. Diarra alitangaza kujiuzulu yeye na baraza lake la mawaziri, kufuatia kukamatwa kwake na wanajeshi, ambao inaripotiwa kuwa walikasilishwa na mienendo yake ya kuwa na uhuru kimawazo, na kuendesha uhusiano wa kisiasa usioruhusiwa.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuteuliwa, Diango Sissoko alisema kipaumbele cha serikali yake kitakuwa kuikomboa sehemu ya kaskazini mwa nchi ambayo inadhibitiwa na wapiganaji wa kiislamu.

''Nataka kuwaambia raia wa Mali kwamba hawana budi kuwa na umoja , kwa sababu watu wakiungana ndipo wanapoweza kuyakabili matatizo'', alisema Sissoko, na kuongeza kuwa ananuia kuunda serikali ya umoja wa taifa.

Jeshi laonywa

Kujiuzulu kwa mtangulizi wake, Cheick Modibo Diarra kulifuatiwa na lawama kutoka jamii ya kimataifa, huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitishia kuliwekea vikwazo jeshi la Mali, ambalo lilisema limemfukuza kutokana na tofauti za kisiasa.

Cheick Modibo Diarra, Waziri Mkuu aliyejiuzulu
Cheick Modibo Diarra, Waziri Mkuu aliyejiuzuluPicha: AP

Wito pia ulitolewa na Marekani, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS kulitaka jeshi la nchi hiyo kuacha kujiingiza katika masuala ya kisiasa. Pande hizo pia zilitishia kuwawekea vikwazo maafisa wa jeshi hilo, ambao zilisema wanakwamisha mchakato wa kurejesha utawala wa katiba.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani Voctoria Nuland alisema hatua zilizochukuliwa dhidi ya Diarra ambaye pia anao uraia wa Marekani, ni kizingiti katika kipindi cha mpito.

Wito wa maridhiano

Mzozo huu mpya nchini Mali unaibuka kukiwa na hali ya kutatanisha juu ya mpango wa kuvituma vikosi vya kigeni kupambana na wanamgambo wa kiislamu walioiteka sehemu ya kaskazi. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky amesema Katibu Mkuu wa Umoja Huo Ban Ki-moon amesikitishwa na hali inayoendelea nchini Mali.

Siku moja kabla ya Cheick Modibo Diarra kujiuzulu, Umoja wa Ulaya ulikuwa umeidhinisha mpango wa kuwapeleka maafisa 250, ambao wangetoa mafunzo kwa jeshi la Mali katika juhudi za kulikomboa eneo la kaskazini. Ingawa msemaji wa Kapteni Amadou Sanogo, kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22, amesema kuondolewa kwa Diarra sio mapinduzi mengine, wachambuzi wanasema ni wazi kwamba kiongozi huyo alishurutishwa kuachia madaraka.

Eneo kubwa kaskazini mwa Mali linadhibitiwa na wanamgambo wa kiislamu
Eneo kubwa kaskazini mwa Mali linadhibitiwa na wanamgambo wa kiislamu

Mchambuzi Samir Gadio mwenye makazi mjini London amesema madhumuni ya kumuondoa madarakani Cheick Modibo Diarra yalikuwa ni kukwamisha mpango wa kutumwa kwa kikosi cha ECOWAS, ambako bila shaka kungeyapunguza madaraka ya Kapteni Sanogo na washirika wake.

Ufaransa na Umoja wa Ulaya zimetoa wito wa kuteuliwa kwa mtu atakayekubaliwa na pande zote nchini Mali, huku Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ikitaka serikali mpya iwe na uwakilishi wa matabaka yote ya kisiasa nchini Mali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA/AFP

Mhariri: Josephat Charo