1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazambia wapiga kura kumchagua rais wao

20 Januari 2015

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa leo(20.01.2015) nchini Zambia katika uchaguzi wa rais ambapo hakuna hakika nani atakuwa mshindi baada ya mvutano wa kuwania madaraka baada ya kifo cha rais Michael Sata mwaka jana.

https://p.dw.com/p/1EN7o
Sambia Wahlkampf Januar 2015
Mdahalo wa wagombea wa kiti cha urais nchini ZambiaPicha: Reuters/R. Ward

Wagombea wawili wa juu ni waziri wa ulinzi Edgar Lungu, mwenye umri wa miaka 58, anayewakilisha chama tawala cha Patriotic Front , na mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema, mwenye umri wa miaka 52 wa chama cha United Party for National Development UPND.

Wanawania muhula uliobaki wa mwaka mmoja na nusu katika kipindi cha uongozi wa marehemu Sata cha miaka mitano katika nchi hiyo ya pili duniani kwa uzalishaji wa madini ya shaba, ambako ushuru mpya kuhusiana na madini hayo umekuwa kwa mshangao mada kuu katika uchaguzi huo.

Sambia Wahlkampf Januar 2015
Waungaji mkono wa chama cha upinzani cha UPNDPicha: Reuters/R. Ward

Mada ya kampeni ya uchaguzi

Chama cha Lungu kilianzisha ushuru huo mwezi Januari mwaka jana, wakati Hichilema ameahidi kuiondoa, akiahidi kuiweka Zambia katika hali ya kuvutia kibiashara.

Mahasimu hao, Lungu ambaye ni mwanasheria na Hichilema ambaye ni mfanyabiashara, akitambulika kama HH wamewavutia watu wengi katika mikutano yao ya mwisho ya kampeni.

Lakini kutokana na kutokuwapo uchunguzi wa maoni, wadadisi wanashindwa kupima ahadi zao. "Ni mbio za watu wawili," amesema Oliver Saasa, mwenyekiti mtendaji wa Premier Consult, shirika la kutoa ushauri katika masuala ya biashara na uchumi. Ni dhahiri kwamba uchaguzi huu utakuwa wa vuta nikuvute , ameongeza.

Wazambia ambao wamechoshwa na uchaguzi, ambao walipiga kura katika chaguzi ambazo zimemuingiza madarakani Sata miaka mitatu iliyopita na wanatakiwa tena kupiga kura mwakani, wamekuwa katika mistari mirefu mapema leo asubuhi katika hali ya hewa ya baridi kali.

Sambia Wahlkampf Januar 2015
Mgombea wa chama cha UPND Hakainde HichilemaPicha: Reuters/Ward

Mvua kubwa yanyesha

Muda mfupi baada ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa mvua ilianza kunyesha kwa wingi mjini Lusaka, lakini haikuwazuwia wapiga kura. Akisimama katika mvua nguo zake zikiwa zimelowana na kukiwa na matope, bila mwanvuli ama koti la mvua, mfuasi wa chama tawala cha PF Allan Kabwe hakukata tamaa.

"Nafahamu watu wengi wanavunjika moyo, lakini baada ya kukamilisha upigaji kura, nitakwenda nyumba kwa nyumba kuwahimiza watu waje kupiga kura. Ni lazima tumuweke Edgar ikulu," amesema kijana huyo wa miaka 24 mchuuzi wa mitaani.

"Ni yangu matumaini kwamba wafuasia wa chama cha upinzani cha UPND hawatakuja kupiga kura".

Michael Sata Sambia Präsident Obit
Marehemu Michael Sata aliyefariki dunia Oktoba mwaka janaPicha: picture-alliance/dpa/Meng Chenguang

Chama cha Lungu cha PF kimeingia katika uchaguzi huu kikiwa kinanyufa baada ya mvutano mkali wa kuwania madaraka baada ya kifo cha Sata mwezi Oktoba mwaka jana, miaka mitatu ndani ya kipindi chake cha utawala cha miaka mitano.

Licha ya sera zinazoelekeza katika ukuaji wa uchumi na uchumi imara katika muda wa miaka michache iliyopita , kiasi ya asilimia 60 ya wakaazi wa zambia wapatao milioni 15 wanaishi chini ya mstari wa umasikini, kwa mujibu wa tarakimu za benki kuu ya dunia.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Idd Ssessanga