1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Watumie akili"

Maja Dreyer15 Novemba 2007

Mgomo kama huu haujawahi kutokea katika historia ya shirika la reli la Ujerumani. Hadi Jumamosi asubuhi waendeshaji wa treni wanapanga kutofanya kazi na hivyo kusimamisha usafiri wa reli nchini kote.

https://p.dw.com/p/CHRe
Treni zimesimamishwa nchini Ujerumani
Treni zimesimamishwa nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/ dpa

Mgogoro juu ya mishahara umefika kilele chake na tangu kuanza miezi kadhaa iliyopita hakuna mengi yaliyofikiwa. Tusikie kwanza gazeti la “Stuttgarter Nachrichten”:

“Ikiwa mkuu wa shirika la reli anashinda katika mgogoro huu, mkuu wa chama cha waendeshaji treni atalazimika ajiuzulu. Vyovyote vile, bwana huyu anabaki na miaka michache tu kabla ya kustaafu. Hata hivyo, yeye anajitolea sana katika mapambano haya ambayo si ya kiuchumi tu, bali yanamhusu kibinafsi. Anataka jina lake liandikwe katika vitabu vya historia kama mkuu wa chama kidogo cha wafanyakazi kilichowahi kulishinda shirika kubwa. Kwa bahati mbaya, watu wengi wenye vyeo vya juu wanapigania kujipatia umaarufu kama huu kabla ya kustaafu bila ya kujali ikiwa mapigano hayo yanawaathiri watu wengine. Bora basi, viongozi hao wote wawili wajiuzulu!”

Moja kwa moja tuendelee na gazeti la “Frankfurter Allgemeine” ambalo limeandika:

“Marubani wa ndege waliupata na madaktari pia, sasa waendeshaji wa treni wanautaka vilevile mkataba wa mishahara kwa jumuiya yao. Mahakama pia imewahakikishia haki ya kufanya mgomo. Mgogoro huu umefika mbali, na sasa shirika la reli litaatharika si tu kupoteza abiria bali kuhusu mustakabali wake. Inabidi basi shirika liwape waendeshaji hao mkataba huo.”

Mhariri wa “Nordbayerischer Kurier” anakumbusha juu ya mpango wa shirika la reli kuuza hisa zake kwenye soko la hisa. Basi anachambua hivi mgomo huu:

“Mgogoro huu hauhusu tu shirika la reli au Ujerumani peke yake. Wafanyakazi wa serikali – kama vile tunavyoweza kuona huko Ufaransa hivi sasa – wanaamini hiyo ni fursa ya mwisho kupigania nyongeza ya mishahara. Wawakilishi kwenye chama cha waendeshaji treni wanajua kwamba shirika hilo la reli hatimaye litabinafsishwa. Kwa hivyo, wanataka mishahara yao iongezwe kabla. Lakini watapoteza kila kita ikiwa wanatumia nguvu kwa namna hiyo, kwani mgomo huu unaweza kuuharibu kabisa usafiri wa reli. Bora watumie akili!”

Na hatimaye katika udondozi huu wa leo ni gazeti la “Reutlinger General Anzeiger”. Mhariri huyu amejihusisha na suala la Pakistan na ameandika hivi:

“Wakati mustakabali wa Afghanistan bado ni wazi, nchi jirani Pakistan inaelekea katika hali hiyo hiyo ya Afghanistan hapo mwaka 1995 ambapo kundi la Wataliban wenye msimamo mkali wa kidini lilipoanza kushinda nchini humo. Pakistan haijawahi kuwa taifa imara. Sasa kuna hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wataliban na wanamgamo wa Kiislamu tayari wanadhibiti maeneo makubwa Kaskazini Magharibi mwa Pakistan. Wakati huo huo, serikali ya Marekani inajitahidi kutayarisha mpango wa kuziokoa silaha za kinyuklia zilizoko Pakistan.”