1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kumi wauawa na waasi mashariki mwa DRC

Iddi Ssessanga
21 Mei 2018

Watu wasiopungua 10 wameuawa na washukiwa wa kundi la waasi wa Uganda ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, katika mauaji ya karibuni zaidi kwenye eneo hilo tete. Makaazi ya watu na biashara pia vimeharibiwa

https://p.dw.com/p/2y3k4
ADF Attacken in Ost-Kongo
Gari lililochomwa wakati wa mashambulizi ya washukiwa wa kundi la ADF mashariki mwa DRC, 20.05.2018. Picha ya John Kanyunyu.Picha: DW/J. Kanyunyu

Afisa wa serikali ya jimbo Donat Kibwana, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kuwa waasi wanaoaminika kutoka kundi la ADF walishambulia kijiji cha Manggboko katika mkoa wa Beni Jumapili usiku, na kuuwa watu 10 wakiwemo wasichana wawili.

Mwandishi wa DW katika mkoa wa Beni John Janyunyu ametembelea familia moja iliyopmpoteza baba mzazi ambapo ameelezea huzunu kutawala katika familia hiyo.

"Na unapoingia Mbau, utaona nyuso za watu zikiwa zimekunjana kufuatia mauaji hayo ya jana jioni katika kata ya Mangboko," ameripoti Kanyunyu.

ADF Attacken in Ost-Kongo
Wakaazi wa Kata ya Mangboko wakiwa katika taharuki kufuatia mauaji yliofanywa na wanaoshukiwa kuwa waasi wa ADF siku ya Jumapili, 20.05.2018. Picha ya John Kanyunyu.Picha: DW/J. Kanyunyu

Jeshi lakwepa wajibu wake

Philippe Paluku Bonane, kiongozi wa kiraia, aliiambia dpa kuwa jeshi halikuingilia kati mauaji hayo hadi waasi walipoondoka kijijini hapo. Mashirika ya kiraia katika wilaya ya Beni, yametangaza siku mbili za maombolezo kuanzia Jumatatu.

Aidha mashirika ya kiraia yametoa mwito kwa serikali kufanya juu chini ili kuhakikisha kuwa mauaji na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF kutoka Uganda yanakomeshwa.

Makundi mbalimbali ya waasi yanaendesha shughuli zake mashariki mwa Congo, yakipigania hasa udhibiti wa rasilimali za eneo hilo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, kundi la ADF liliundwa mwaka 1995 na wanakutikana kwenye eneo la milima mpakani mwa DRC na Uganda. Kundi hilo linafahamika kwa kutumia wanajeshi watoto.

Kundi hilo limeuawa takribani watu 2000 katika mji na Wilaya ya Beni katika kipindi cha miaka minne, ameripoti mwandishi wa DW John Kanyunyu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef