Watu 19 wauawa katika mkanyagano
25 Julai 2010Mkanyagano huo ulitokea kwenye ujia mwembamba kuelekea kwenye uwanja wa tamasha. Hadi sasa haijulikana kilichosababisha kuzuka kwa mkanyagano huo.
Kuna mashahidi wanaosema kuwa watu walibanana katika ujia huo na wengine waliojaribu kuparamia ukuta na ngazi waliporomoka. Waandalizi wa tamasha hilo wanazidi kukosolewa. Zaidi ya watu milioni moja walihudhuria tamasha hilo katika eneo lenye uwezo wa kuchukua robo ya idadi hiyo.
Maafa hayo yamesababisha huzuni na mshtuko mkubwa miongoni mwa umma hapa Ujerumani na katika nchi za nje. Rais wa Ujerumani Christian Wulff amesema fikra zake zipo kwa wahanga wa ajali hiyo,familia zao na marafiki zao. Vile vile ametoa mwito wa kufanywa uchunguzi wa kina kuhusu maafa hayo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel pia wametoa pole kwa familia za wahanga.
Waziri Mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia, Hannelore Kraft akiwa katika hali ya huzuni alitoa rambirambi kwa familia za wahanga na amesema, wale waliojeruhiwa watashughulikiwa ipasavyo. Halikadhalika Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, José Manuel Barroso ametoa rambirambi zake kwa familia zilizofiwa kutokana na mkanyagano uliotokea katika tamasha la muziki "Love Parade" nchini Ujerumani.
Mwandishi: P.Martin/dpa
Mhariri: M.Dahman