1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 12 wauawa na wengine 26 kujeruhiwa Basra

Kalyango Siraj25 Machi 2008

Kiongozi wa kidini atisha kuitisha mgomo wa kitaifakupinga mashambulio

https://p.dw.com/p/DUFZ

Kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Kishia nchini Iraq Moqtada al-Sadr ametishia kuitisha uasi wa raia wa kutotumia nguvu dhidi ya serikali,kufuatia kutokea mapigano kati ya wanamgambo wa dhehebu lake dhidi ya vikosi vya serikali katika mji wa kusini wa Basra ambapo watu kadhaa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Tisho la kiongozi huyo wa kidini amelitoa katika taarifa yake iliosomwa mjini Najaf na mjumbe wake Hazam al-Aaraji.

Katika taarifa hiyo Sadr,amewahimiza raia wa Iraq kufanya mgomo wa nchi nzima wa kukaa nyumbani.Mwito huo umefuatia operesheni inayofanywa na vikosi vya serikali ya Iraq vikijaribu kuyadhibiti makundi ya wanamgambo katika mji huo ambao wengi ni wa kundi la Mahdi la Sadr.Sadr amesema hatua kadhaa zitachukuliwa ikiwa hujuma dhidi ya wanachama wake hazitakomeshwa mara moja.

Duru za usalama katika mji huo zinasema takriban watu 12 wameuawa hadi sasa kutokana na mapiganao hayo.Miongoni mwa waliouawa ni raia wa kawaida pamoja na wapiganaji wa kundi la jeshi la Mahdi.Watu wengine 26 ndio wamejeruhiwa hadi sasa wakati mapigano makali yakiwa yanaendelea.

Mapigano,kwa mujibu wa duru za kijeshi katika mji huo, inasemekana yalikuwa makali baada ya wapiganaji wa jeshi la Mahdi kushambulia vituo kadhaa vya kiusalama katika mji huo.

Hata hivyo ofisi ya habari ya Moqtada al-Sadr imekanusha madai ya kuwepo mapigano kati ya vijana wake dhidi ya vikosi vya serikali na badala yake kusema kuwa Sadr amewaamuru vijana wake kutopigana na askari wa serikali bali kuwakabidhi nakala za kitabu kitakatifu kwa waislamu cha Kurani,kama ishara ya amani.

Wanajeshi wapatao 50,000 wa Iraq wakisaidiwa na polisi wako katika kibarua cha kurejesha udhibiti wa mji huo katika mikono ya serikali na vilevile kuwafanya raia kutii sheria.

Mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraq zamani ulikuwa chini ya udhibiti wa jeshi la Uingereza tangu uvamizi wa nchi hiyo uanze mwaka wa 2003. Na mwezi Disemba ulirejeshwa katika mikono ya Iraq .

Lakini haukuwa salama kutokana na mapigano kati ya makundi mbalimbali ya kimgambo ya washia pamoja na magenge mbalimbali katika mji huo.

Serikali ya waziri mkuu Nuri al Maliki imeamua kuchukua hatua sasa ili kuudhibiti mji huo wenye utajiri wa mafuta.Yeye mwenyewe,Wazri mkuu yuko mjini humo akiongoza operesheni hiyo.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kuona hali ya utulivu inarejea ni kutangaza amri ya kutotoka nje usiku.

Kuanzia kesho,jumatano,barabara zote kutoka maeneo jirani kuelekea mji wa Basra zitafungwa kwa mda wakati wa jioni hadi ijumaa.

Shule za upili mkiwemo vyuo vikuu, nazo zimefungwa kuanzia leo jumanne hadi alhamisi.

Ndege kadhaa za kijeshi za Marekani zimeonekana zikitua katika uwanja wa ndege wa Basra.