1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 1,000 wakamatwa Ethiopia

Mohammed Khelef
19 Oktoba 2016

Watu 1,000 wametiwa nguvuni na vyombo vya dola nchini Ethiopia kufuatia ghasia zinazohusishwa na maandamano dhidi ya serikali yaliyochanganyika na mauaji na uharibifu wa mali, huku hali ya hatari ikiimarishwa.

https://p.dw.com/p/2RPzy
Ethiopia State of Emergency Merkel (picture alliance / AP Photo)
Picha: picture-alliance/AP Photo

Meya wa mji wa Sebeta, ulio kando mwa mji mkuu Addis Ababa, Ararsa Merdesa, ameliambia shirika la habari la Marekani, Associated Press, kwamba licha ya baadhi ya watu hao 1,000 wameachiliwa, wengi wao bado wamo mikononi mwa vyombo vya usalama. Mji huo ndio ulioshuhudia viwanda na magari kadhaa yakichomwa moto wakati wa maandamano ya kuipinga serikali. 


Kwa mujibu wa meya huyo, ni 50 tu kati ya watu waliokamatwa ambao walikuwa wenyeji wa mji huo, huku waliobakia wakiwa watu "waliokuja kufanya ghasia". Ghasia hizo zilitokea baada ya zaidi ya watu 50 kufariki dunia kwenye mkanyagano uliotokea pale polisi ilipotumia gesi ya machozi kuwachawanya waandamanaji kwenye mkoa wa Oroma.

Taifa hilo la mashariki mwa Afrika lilitangaza hali ya hatari mwezi huu baada ya takribani mwaka mzima wa maandamano, ambayo baadhi ya wakati yaligeuka makabiliano na mauaji, kati ya waandamanaji wanaopigania haki zaidi za kibinaadamu na kiuchumi na vyombo vya dola. Waandamanaji wamekuwa wakilenga vitega uchumi wanavyovituhumu kuwa na mafungamano na serikali, vikiwemo vile vinavyomilikiwa na wawekezaji wa kigeni.

Upinzani wasema hali ya hatari ni kisingizio

Katika mzungumzo yake na DW kwa njia ya simu, kiongozi wa upinzani nchini humo, Merara Gudina, amesema hali hiyo ya hatari ni kisingizio tu cha serikali kuendeleza ukandamizaji wake. "Serikali iko kwenye hali mbaya sana kabisa kuwahi kuitokezea tangu iingie madarakani mwaka 1991. Takribani kote nchini watu wanaupinga utawala, ndio maana inatangaza hali hii ya hatari. Lakini kwa ujumla si jambo geni, kwani tangu zamani imekuwa ikitumia njia hii kwa kipindi kirefu kufanya mauaji ya ovyo ovyo, kuweka watu ndani. Si jambo geni."

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International linasema kiasi watu 600 wameshauawa tangu Novemba mwaka jana hadi sasa na wengine 200 kwenye mkoa wa Amhara. 

Mtafiti wa shirika jengine la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch nchini Ethiopia, Felix Horne, anasema ndani ya kipindi cha miezi 11, vyombo vya usalama vimeshawauwa mamia ya waandamanaji, kuwatia nguvuni maelfu kadhaa na huku vikiwatendea sivyo wale waliomo mikononi mwao. Kwa mujibu wa Horne, jumla ya mambo hayo ndiyo yaliyozusha hasira miongoni mwa raia, na kwamba ghadhabu hiyo sasa imesambaa kote.

Hapo Jumapili, serikali iliimarisha hali yake ya hatari kwa kupiga marufuku upatikanaji wa taarifa za vyombo vya habari vya nje ambavyo vinaelemea upinzani na pia kuwazuwia mabalozi kutembea umbali wa kilomita 40 nje ya mji mkuu, Addis Ababa, kwa kile ilichosema ni kwa usalama wao. 

Moja ya hatua hizo mpya ni pamoja na marufuku ya kubeba silaha katika eneo lenye ukubwa wa 50 katika mpaka wa nchi hiyo, huku vyama vya upinzani vimepigwa marufuku kutotoa taarifa kupitia vyombo vya habari, ambazo zinachochea vurugu na viongozi wa dini nao wamezuiwa kutoa kauli ambazo zinahusiana na siasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Phillip Sandner
Mhariri: Daniel Gakuba 

Äthiopien Proteste Gebet
Sala ya kuwaombea waandamanaji waliouawa kwenye mji wa Bishoftu karibu na mjii mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, tarehe 9 Oktoba 2016.Picha: Reuters/T. Negeri