1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto milioni 700 wapokonywa utoto wao

Daniel Gakuba
1 Juni 2017

Ripoti ya shirika la wahisani la Save the Children inasema kuwa watoto milioni 700 duniani wamepoteza fursa ya utoto wao, kutokana na sababu mbali mbali kama magonjwa, ndoa za mapema na mizozo katika maeneo wanayoishi.

https://p.dw.com/p/2dxDm
Indien Steinbrucharbeiter Arbeitssicherheit
Watoto wengi wanafanyishwa kazi nzito badala ya kupelekwa shulePicha: Getty Images/AFP/C. Mao

 

Ripoti hiyo ya Save the Children ambayo ilitolewa Jumatano jioni, imeziorodhesha nchi 172 kulingana na kiwango cha ubora wa maisha ya watoto katika nchi hizo, na saba kati ya kumi zilizoko mkiani zinapatikana katika Ukanda wa Magharibi na Katikati mwa Afrika. Nchi hizo kumi ambako watoto wana matatizo makubwa ni Guinea,  Sierra Leone, Burkina Faso,  Sudan Kusini na Chad. Nyingine ni Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali,  Angola na Niger iliyo mkiani kabisa. Kwa upande mwingine Norway, Slovania na Finland ndizo zinazoongoza kwa kuwa na mazingira bora kwa watoto.

Wengi wa watoto milioni 700 wanaoathirika wanaishi katika nchi zilizoachwa nyuma kimaendeleo, ambako huduma za afya na elimu ni duni, na kuna ukosefu wa teknolojia iliyoboresha maisha ya watoto kwingineko.

Mkurugenzi mkuu wa Save the Children Helle Thorning-Schmidt ameliambia shirika la Thompson Foundation kwamba watoto wengi katika maeneo hayo wanazongwa na mseto wa shida za umasikini na kubaguliwa, ambazo zinakosesha kuishi kama watoto.

Takwimu za kuogofya

Libanon Syrische Flüchtlinge
Watoto milioni 28 wameyakimbia makazi yaoPicha: Reuters/Ali Hashisho

Save the Children inasema katika ripoti yake hiyo kuwa watoto milioni 263 wenye umri wa kwenda shule hawasomeshwi, kiwango hicho kikiwa sawa na mtoto mmoja kati ya sita duniani. Idadi kubwa ya watoto wasio mashuleni inapatikana katika mataifa ya Asia Kusini.

Inakadiria pia kuwa watoto milioni 168 wanafanyishwa kazi nzito, nusu yao wakifanya kazi zenye hatari kubwa kama kuchimba madini migodini, utumishi katika viwanda vya nguo, na kuokotaokota vitu katika majalala.

Aidha, nusu ya wato wote wenye umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa katika ukuaji wao kutokana na utapiamlo. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki Tanzania imewekwa katika kundi hilo, ripoti hii ikionyesha kuwa asilimia 34 ya watoto wote nchini humo hawakui ipasavyo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia imo katika kundi hilo, matatizo ya udumavu yakiathiri asilimia 43 ya watoto.

Kuozwa wakiwa watoto

Schwangeren Bauch
Mamilioni ya watoto wanatiwa ujauzito kabla ya kutimiza miaka 20Picha: Fotolia/Andres Rodriguez

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kadhia ya ndoa za utotoni inawasibu watoto wa kike milioni 15 kila, milioni 4 kati ya hao wakiolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.

Matatizo mengine mabaya yanayowakumba watoto yanatokana na mizozo, ambayo imesababisha wapatao milioni 28 kuyahama makazi yao. Watoto 75,000 wa chini ya miaka 20 waliuawa mnamo mwaka 2015 pekee, kulingana na ripoti hii.

Ripoti hiyo inazitaka nchi husika kuondoa sera na desturi zenye ubaguzi, na kuwekeza rasrimali zaidi katika huduma za jamii, kama ilivyokubaliwa katika malengo ya milenia ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa.  Malengo 17 ya maendeleo endelevu yanayoazimia kumaliza umasikini wa kupindukia ifikapo mwaka 2030, yalitoa ahadi ya kuwajali kwanza wale wenye mahitaji makubwa, ili kuepuka kuziacha nyuma jamii dhaifu.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba /rtre,DW,

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

http://www.savethechildren.org/site/c.8rKLIXMGIpI4E/b.6153061/k.7E4A/Publications_and_Reports.htm