1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watekaji nyara watishia kumuua msichana mdogo wanayemzuilia

Josephat Charo6 Julai 2007

Watu waliokuwa wamejihami na bunduki waliomteka nyara msichana wa umri wa miaka mitatu raia wa Uingereza kusini mwa Nigeria, wamesema watamuua msichana huyo ikiwa babake hatajisalimisha kwao na kuchukua mahala pake.

https://p.dw.com/p/CHBQ
Picha ya mwanamgambo wa kundi la waasi nchini Nigeria
Picha ya mwanamgambo wa kundi la waasi nchini NigeriaPicha: AP

Oluchi Hill, mama wa Margaret Hill, msichana mdogo aliyetekwa nyara kusini mwa Nigeria amesema leo kwamba watekaji nyara wametaka amtoe mumewe ili wamrudishie msichana wake. Oluchi pia amesema waasi hao walimpigia simu kupanga mkutano na kutaka mumewe ajisalimishe.

Kufikia sasa hajaweza pamoja na polisi kufaulu kuufikia mji katika jimbo la Bayelsa kwenye eneo la Niger Delta, ambako mkutano huo ulitarajiwa kufanyika. Hata hivyo amesema amefaulu kuzungumza na msichana wake aliyekuwa akilia. Tangia wakati huo, mama huyo hajakuwa na mawasiliano yoyote na watekaji nyara hao.

Margaret Hill alitekwa nyara jana katika mji wa Port Harcourt katika jimbo la kusini la Rivers wakati alipokuwa akipelekwa shuleni. Duru za polisi zinasema watekaji nyara wanaomzuilia msichana huyo walipiga simu saa chache baadaye kusema alikuwa salama.

Watekaji nyara hao walitishia kumuua msichana huyo kama babake hangekwenda kukutana nao katika kipindi cha saa tatu. Oluchi Hill amesema mumewe alitaka kwenda kumchukua msichana wake lakini kamanda wa polisi akamzuilia asifanye hivyo.

Wizara ya mashauri ya kigeni nchini Uingereza imetaka msichana huyo aachiliwe huru mara moja.

Kundi kuu la waasi katika eneo lililo na mafuta mengi la Niger Delta nchini Nigeria, MEND, limelaani vikali utekaji nyara wa msichana huyo huku juhudi za kumuokoa zikiendelea kufanywa na maafisa wa serikali. Jomo Ngomo, msemaji wa kundi hilo, amesema utekaji nyara wa msichana huyo ni kitendo cha kuchukiza sana. Aidha ameahidi watawasaka waliomteka nyara msichana huyo na kutoa adhabu kwa wakati unaofaa.

Kundi la waasi la MEND linaelezwa kuwa kundi lililo na silaha za kisasa na lililojiimarisha zaidi kuliko makundi mengine ya waasi yanayojihusiaha na utekaji nyara katika eneo la Niger Delta. Mapema wiki hii kundi hilo lilitangaza kumalizika kwa usitishwaji wa mapigano wa miezi minne ulioitishwa ili kutoa mwanya yafanyike mazungumzo baina ya waasi wa kundi hilo na serikali ya Nigeria.

Baadhi ya wanamgambo wa eneo la Niger Delta wanasema wanapigania pato la mauzo ya mafuta liwanufaishe wakaazi wa eneo hilo, ingawa kuna makundi yaliyojihami na silaha ambayo huwateka nyara watu ili yapate pesa. Wafanyikazi 200 wa kigeni wa makampuni ya mafuta wametekwa nyara katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwaka jana. Wengi wao wamekuwa wakiachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa siku au majuma kadhaa na kila mara fedha hulipwa watekaji nyara.

Utekaji nyara wa Margaret Hill ulifanyika yapata saa 24 baada ya wafanyikazi wa kampuni ya mafuta ya kigeni kutekwa nyara katika eneo la Soku kwenye jimbo la Rivers. Mwezi Mei mwaka huu, mtoto mwingine, ambaye uraia wake haukujulikana, alitekwa nyara na kuachiliwa huru siku nne baadaye.