1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wateka nyara watishia tena kuwaua wajerumani wanaowashikilia nchini Irak

3 Aprili 2007

Wateka nyara wanaowashikilia wajerumani wawili nchini Irak kwa mara nyingine wameipa Ujerumani muda wa siku kumi kuondoa majeshi yake kutoka Afghanistan la sivyo wajerumani hao watauliwa.

https://p.dw.com/p/CHGz
Picha: AP

Wateka nyara hao wametoa tishio hilo kwenye tovuti kuishurutisha Ujerumani ianze kuondoa majeshi yake kutoka Afghanistan.Iwapo serikali ya Ujerumani haitafanya hivyo , magaidi hao wamesema kuwa watawaua wajerumani hao .

Magaidi hao wametoa tishio lao wakati ambapo bunge la Ujerumani limepitisha uamuzi wa kupeleka ndege aina ya Tornado zitakazofanya kazi ya doria nchini Afghanistan.

Ndege hizo zitaimarisha kazi ya wanajeshi alfu tatu wa Ujerumani waliopo nchini humo kama sehemu ya jeshi la kimataifa la kulinda amani.Licha ya upinzani kutoka kwa chama cha mlengo wa kushoto kwenye bunge uamuzi wa kupeleka ndege hizo umepitishwa .

Akizungumzia juu ya uamuzi huo waziri wa ulinzi wa Ujerumani bwana Franz Joseph Jung ameeleza kuwa ndege hizo zimepelekwa kuitikia ombi la NATO juu ya kuziba pengo lililopo katika mfumo wa doria nchini Afghanistan.

Wateka nyara wanaowashilikia wajerumani hao wawaili wanataka wanajeshi hao alfu tatu wa Ujerumani waanze kuondoka nchini Afghanistan katika kipindi cha siku kumi.

Wajerumani hao, bibi Hanelore Krause mwenye umri wa miaka 61 na mwanawe mwenye umri wa miaka 2o walitekwa nyara mwanzoni mwa mwezi februari mjini Baghdad. Wakati huo magaidi hao pia waliipa serikali ya Ujerumani muda ili kuanza kuondoa majeshi yake kutoka Afghaistan na pia walitishia kuwaua mateka wao.

Baada ya ukimya wa wiki kadhaa wateka nyara hao wametoa ukanda mwingine wa video kwenye tovuti kuitaka Ujerumani iondoe majeshi yake kutoka Afghanistan katika kipindi cha siku kumi la sivyo watawaua wajerumani wanaowashikilia.

Lakini serikali ya Ujerumani imesema kuwa haitakubali kushurutishwa na magaidi. Hatahivyo serikali hiyo inafanya juhudi ili kuokoa maisha ya mateka hao.

Na ABDU MTULLYA