1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watalii waanza kuondoka Thailand, baada ya kukwama kwa siku tatu katika Viwanja vya Ndege.

Halima Nyanza28 Novemba 2008

Maelfu ya watalii, waliokwama katika viwanja vya ndege nchini Thailand, vilivyozingirwa na wapinzani wa serikali ya nchi hiyo, leo wameanza kuondoka, kwa kutumia Uwanja wa kambi ya Jeshi iliyotumiwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/G40l
Wapinzani nchini Thailand, ambao wanashinikiza serikali ya nchi hiyo kuondoka madarakani, na kuitisha uchaguzi mpya.Picha: AP


Maelfu ya watalii hao, walikwama viwanjani humo toka siku ya Jumanne, baada ya wapinzani hao wa serikali, kuzingira uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi, katika juhudi zao za kuishinikiza serikali kuondoka madarakani na kuitisha uchaguzi mpya.

Jana wakuu wa viwanja vya ndege nchini humo walitoa ruhusa kwa mashirika ya ndege kutumia Uwanja wa Ndege wa Kambi hiyo ya Jeshi la Wanamaji, iliyokuwa ikitumiwa na Jeshi la Marekani, wakati wa vita vya Vietnam, iliyo karibu kilomita 190 kusini mashariki, mwa mji mkuu wa nchi hiyo Bangkok, na kwamba tayari ndege kadhaa zimekwisha tua hadi leo.

Baadhi ya Makampuni ambayo yamethibitisha leo kutuma ndege katika uwanja huo wa Kijeshi ni pamoja na Malaysia, Singapore na Taiwan.

Shirika la ndege la Korea kusini, tayari lilituma ndege maalum jana na kwamba abiria wengine watachukuliwa leo.

Leo Waziri wa Utalii nchini humo, aliitisha kikao cha dharura ambacho kimehudhuriwa na maafisa wa Viwanja vya ndege na wawakilishi kutoka mashirika 50 ya ndege, kujaribu na kupanga mikakati ya kuweza kuwatoa na kuingiza watu nchini humo.

Hatua hiyo, iliyochukuliwa na wapinzani nchini humo, ya kuzingira viwanja vya ndege imeelezwa kuathiri zaidi uchumi, hususan katika sekta ya Uwekezaji.

Katika hatua nyingine Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNIFEC, limesema linawasiwasi na usalama wa watoto waliokuwa katika viwanja hivyo vya ndege na kuwataka viongozi wanaoendeleza upinzani huo kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa salama.

Waziri Mkuu wa Thailand Somchai Wongssawat ametangaza hali ya hatari katika viwanja hivyo vya ndege, lakini hata hivyo Jeshi nchini humo linahofiwa kwamba shambulio lolote linaweza kusababisha makabiliano ya umwagaji namu na wapinzani, wakati ambao mazungumzo kuweza kujaribu kumaliza tatizo hilo yakiendelea.

Polisi nchini humo wamekuwa wakifanya mazungumzo na wapinzani hao, lakini hata hivyo Kamanda wa polisi anayeongoza majadiliano hayo, amesema watachukua hatua zaidi iwapo mazungumzo hayo yatashindwa.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na wapinzani hao wafuasi wa chama cha People's Alliance of Democracy, ya kuzingira Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Don Muang na ule wa Suvarnabhumi kumefanya kuvunjika kwa mawasiliano katika sekta hiyo ya anga kati ya mji wa Bankok na dunia, kuacha maelfu ya wasafiri kukwama na kuathiri utalii, ambao unategemewa katika uchumi wa nchi hiyo.