1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban 50 wauawa Afghanistan

12 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CafN

KABUL.Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imesema kuwa zaidi ya wanamgambo 50 wa kitaliban wameuawa katika siku mbili za mapigano makali kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji hao huko katika jimbo la kusini la Musa Qala.

Mjini Washington Waziri wa Ulinzi wa Marekani Roberts Gates amesema kuwa ni lazima kwa nchi nyingine wanachama wa NATO kushiriki katika harakati za kijeshi huko Afghanistan.

Gates aliiambia kamati ya ulinzi ya bunge la wawakilishi la Marekani kuwa ghasia na vurugu zimeongezeka nchini Afghanistan toka majeshi ya NATO yalipochukua jukumu la ulinzi nchini humo mwaka 2006.

Amesema kuwa anapanga kuwa na majadiliano na mawaziri wa ulinzi wa nchi zilizo na vikosi huko Afghanistan, wiki hii nchini Scotland.

Maafisa wa Marekani wamekuwa wakitaka nchi nyingine katika muungano wa nchi 26 za NATO kuongeza vikosi zaidi na wakufunzi wa kijeshi na polisi huko Afghanistan katika kipindi hiki ambacho mkazo mkubwa kijeshi wa Marekani unaelekezwa Iraq.