1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watalaamu wautathmini uharibifu wa Palmyra

Mjahida 28 Machi 2016

Wanajiolojia au wataalamu wa mambo ya kale wameelekea mjini Palmyra kutathmini uharibifu uliofanywa na wanamgambo wa IS baada ya kuondolewa na vikosi vya serikali ya Syria mjini humo katika mapambano makali.

https://p.dw.com/p/1IKoO
Syrien Palmyra UNESCO Weltkulturerbe - Rückeroberung durch syrische Armee
baadhi ya majengo katika mji wa kale wa PalmyraPicha: Getty Images/AFP/M. Al Mounes

Kulingana na muandishi habari wa shirika la AFP mjini Palymra, minara kadhaa na majengo vimeharibiwa, mwaka mmoja baada ya wanamgambo hao kuuteka mji huo, huku akisema maeneo mengine mengi ya mji huo yalikuwa salama.

Aidha Maeneo ya watu karibu na mji huo uliyokuwa na idadi ya watu 70,000 kabla ya vita, ulikuwa mtupu huku athari za mapigano zikionekana wazi katika eneo hilo.

"Tulitarajia uharibifu mkubwa kuliko huu tunaouona lakini baadhi ya maeneo mengi yako salama tu, tungeupoteza mji mzima wa Palmyra lakini hilo halikufanyika, furaha ninayoisikia haiwezi kuelezeka,"alisema Maamoun Abdulkarim mtaalamu wa mambo ya kale wa Syria.

Syrien Palmyra Syrische Armee erobert Zitadelle
Wanajeshi wa Syria baada ya kuukomboa mji wa PalmyraPicha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Kwa upande wake shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema wapiganaji takriban 400 wa dola la Kiislamu waliuwawa huku wanajeshi 188 pamoja na wanamgambo waliyotiifu kwa serikali ya Assad wakiuwawa pia katika mapigano yaliyopelekea mji huo kukombolewa na serikali.

Wanajeshi wa Syia, wanamgambo waliyotiifu kwa serikali na wapiganaji wa kutoka Urusi walionekana wakitembea tembea mjini humo bila hofu baada ya kuukomboa hapo jana.

Ndege za Urusi zaripotiwa kuondoka Syria

Katibu wa Baraza la Usalama wa taifa nchini Iran amempongeza rais Bashar al Assad kwa kuukomboa tena mji wa Palymra. Katibu huyo Ali Shamkhani amesema ujasiri wa taifa la Syria, serikali na jeshi lake kukabiliana na ugaidi ni kitu cha kujivunia. Amesema jeshi la Iran litaendelea kuiunga mkono serikali ya Bashar al Assad.

Kwa upande mwengine ndege tatu za kivita kutoka Urusi zimeondoka katika kambi yake nchini Syria kuelekea Moscow,pamoja na wahandisi na wafanyakazi kadhaa wa kiufundi hii ikiwa ni kwa mujibu wa Televisheni ya Taifa nchini Urusi.

Syrien Russische Militärbasis in Latakia
Baadhi ya ndege za Urusi zikiondoka SyriaPicha: Getty Images/AFP

Mwezi huu rais Vladimir Putin aliamuru kuondoka kwa majeshi yake nchini Syria baada ya kuendesha mashambulizi ya angani kwa miezi mitano nchini humo dhidi ya wanamgambo wa dola la Kiislamu. Putin amesema tayari Urusi imetekeleza malengo yake huku akimpongeza rais Assad kwa kuutwaa tena mji wa Palymra.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga