1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu kutumwa DRC kudhibiti Ebola

Amina Mjahid
14 Mei 2018

Serikai ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa wameanza kupeleka wataalamu wa afya nchini Congo, kuzuwia kuenea kwa mripuko wa ugonjwa wa Ebola

https://p.dw.com/p/2xg2Q
Symbolbild Ebola-Ausbruch
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/A. Jallanzo

Kulingana na Mkurugenzi wa Afrika wa shirika la afya duniani WHO Matshidiso Moeti, wamepata dozi 4000 za chanjo ya majaribio ya Ebola, na wanajitayarisha kuipeleka nchini Congo wiki hii. Shirika hilo linatarajia kuanza kampeni ya chanjo ya ebola katika eneo la Bikoro, lililoko karibu na mpaka wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Moeti amesema watu 362 wamebainika kuwa na mawasiliano na wagonjwa, hali inayotilia mkazo umuhimu wa kupelekwa kwa chanjo ya ebola nchini humo haraka iwezekanavyo. Ameongeza kuwa wawili kati ya watu hao walifika katika mji wa Mbandaka. Wasiwasi mkubwa zaidi tangu kuripotiwa kwa mripuko huo umekuwa juu ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika mji huo.

Kuba Ebola Trainingslager
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Perez/Cubadebate

"Tuna wasiwasi maana huu ni  mji ulio na idadi ya watu milioni moja," alisema Matshidiso Moeti alipokuwa akizungumza na shirika la habari la Reuters.

Kisa cha hivi karibuni cha maambukizi ya ugonjwa huo kiliripotiwa siku ya Ijumaa Kaskazini Magharibi mwa jimbola Equateur lililotembelewa na Waziri wa Afya Oly Ilunga Kalenga siku ya Jumamosi akiwa pamoja na maafisa wengine kutoka WHO na shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.

Gianfranco Rotigliano, kaimu mwakilishi wa shirika hilo la UNICEF katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema watashughulikia kuwepo kwa maji safi, kuwahamasisha watu kuosha mikono na kuhakikisha kunakuwepo na vituo vya huduma ya afya vya kutosha.

Serikali na maafisa wa Mashirika ya yasio ya kiserikali wako mbioni kuudhibiti ugonjwa wa ebola

Congo iliripoti kisa cha kwanza cha ugonjwa wa ebola katika kijiji cha Ikoko Impenge karibu na mji wa Bikoro siku ya Jumanne huku watu 32 wakiambukizwa pamoja na kuripotiwa  vifo 18 tangu Aprili 4. Hata hivyo baadhi ya vifo vilivyotokea mapema mwezi wa Januari havija husishwa na ugonjwa wa ebola.

Kongo Ausbruch von Ebola
Picha: Imago/Nature Picture Library

Aidha maafisa wa kwa sasa wanajitahidi kuuzuwiya ugonjwa huo kuenea  kwa kasi kama ilivyotokea Magharibi mwa Afrika mwaka 2014 hadi 2016 wakati ebola iliposababisha vifo ya zaidi ya watu 11,300 nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Ugonjwa huo unaosababisha kuvuja damu ndani na nje ya mwili kutokana na kuathirika kwa mishipa ya damu, tayari umeshasambaa katika maeneo matatu tofauti katika jimbo la Equateur, Mbandaka, Bikoro na Iboko, hali inayoziweka nchi tisa jirani na Congo katika tahadhari ya hali ya juu iwapo ugonjwa huo utavuka mipaka na kuingia Jamhuri ya Congo au Jamhuri ya Afrika ya kati.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga