1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi licha ya silaha za nyuklia kupungua

15 Juni 2015

Ripoti iliyotolewa leo (15.06.2015) na Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa amani, SIPRI, imesema mataifa yanayomiliki sihala za nyuklia yameendelea kuimarisha silaha zao licha ya juhudi zinazofanywa kuziangamiza.

https://p.dw.com/p/1FhM3
Pakistan testet atomwaffenfähige Raketen
Picha: picture alliance / dpa

Ripoti ya mwaka huu ya taasisi ya SIPRI imesema kati ya mwaka 2010 na 2015 idadi ya vichwa vya nyuklia ilipungua kutoka 22,600 hadi 15,850, huku Marekani na Urusi zikipunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya silaha zao. Taasisi hiyo pia imedokeza kuhusu mipango mipana ya kisasa na ya gharama kubwa ya kuimarisha utengenezaji wa silaha za nyuklia katika mataifa hayo mawili makubwa yanayomiliki asilimia 90 ya silaha za nyuklia duniani.

Mtafiti wa taasisi ya SIPRI yenye makao yake mjini Stockholm nchini Sweden, Shannon Kile amesema katika taarifa yake, "Licha ya nia ya jumuiya ya kimataifa kuzipa kipaumbele juhudi za kupunguza na kuziangamiza silaha za nyuklia, mipango ya kuimarisha mifumo ya kutengeneza silaha hizo kuwa ya kisasa inapendekeza kwamba hakuna nchi yoyote itakayoachana na silaha zake za nyuklia katika siku zijazo."

Kwa mujibu wa taasisi ya SIPRI mataifa mengine matatu yanayomiliki silaha za nyuklia yanayotambuliwa kisheria na mkataba wa mwaka 1968 wa kudhibiti kusambaa kwa silaha hizo, zinatengeneza au kutumia mifumo mipya ya kutengeneza silaha za nyuklia au zimetangaza nia yao kufanya hivyo. Nchi hizo tatu ni China, yenye vichwa 260 vya nyuklia, Ufaransa ikiwa na vichwa 300 vya nyuklia na Uingereza, ambayo ina vichwa 215 vya nyuklia.

Mwanzo wa mashindano ya silaha?

China ni nchi pekee kati ya mataifa matano yenye silaha za nyuklia duniani kuongeza kwa kiwango cha wastani silaha zake.

Infografik Stand der Atomwaffenarsenale weltweit 2015 Englisch
Ramani inayoonyesha silaha za nyuklia duniani

Huku mataifa mengine yanayomiliki silaha za nyuklia yakiwa na kiwango kidogo cha silaha hizo, India na Pakistan zinaendelea kuongeza silaha zao huku Israel ikiwa imefaulu kuyafanyia majaribio makombora yake ya masafa marefu. Inaripotiwa India ina vichwa kati ya 90 na 100 vya nyuklia, Pakistan ina vichwa kati ya 100 hadi 120 na Israel ina vichwa 80 vya nyuklia.

Korea Kaskazini inaaminiwa inatengeneza na kuimarisha silaha zake za nyuklia ikiwa na vichwa kati ya sita na vinane, lakini taasisi ya SIPRI imesema ilikuwa vigumu kutathmini ufanisi wa kiufundi uliopatikana.

Taarifa za kuaminika kuhusu silaha za nyuklia zilitofautiana kwa kiwango kikubwa huku Marekani ikiongoza kwa uwazi katika ripoti hiyo, nazo Uingereza na Ufaransa zikisitasita kutoa taarifa na Urusi ikikataa kutoa taarifa rasmi, isipokuwa tu katika mawasiliano na Marekani.

Barani Asia, China haikusema mengi kuhusu silaha zake ya nyuklia na taarifa yoyote iliyotangazwa hadharani na washindani wake, India na Pakistan, ilihusu majaribio ya makombora.

Nchi tano zinazomiliki silaha za nyuklia na ambazo pia wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, yaani Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa, pamoja na Ujerumani, zinafanya mazungumzo na Iran kuishawishi Jamhuri hiyo ya kiislamu iachane na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia ili vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa viondolewe.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP

Mhariri:Iddi Sessanga