1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi kuhusu Kombe la Dunia Qatar 2022

20 Septemba 2013

Qatar imesisitiza kuwa inaweza kuandaa dimba la Kombe la Dunia mwaka wa 2022 katika majira ya joto, hata wakati Shirikisho la FIFA likiendelea kuwekewa mbinyo wa kuhamisha tamasha hilo hadi msimu wa baridi

https://p.dw.com/p/19lFU
Muundo wa Kompyuta wa mojawapo ya viwanja vitakavyotumiwa katika kombe la dunia jijini Doha Qatar 2022
Muundo wa Kompyuta wa mojawapo ya viwanja vitakavyotumiwa katika kombe la dunia jijini Doha Qatar 2022Picha: picture alliance/abaca

Taifa hilo lenye utajiri wa nishati, ambako nyuzijoto hufikia sentigredi 45 ilipewa kibali cha kuandaa Kombe la Dunia miaka mitatu iliyopita katika uamuzi wa kushangaza.

Qatar inasema inaweza kukubali kuhamisha dimba hilo hadi msimu wa baridi lakini ikasisitiza kuwa licha ya joto kali, inaweza kuandaa Dimba la Dunia msimu wa joto kwa kujenga viwanja vyenye hewa ya baridi kwa kutumia teknolojia mpya inayojali mazingira.

Namna ambavyo mashabiki wataweza kukabiliana na joto, nje ya viwanja, bado ni suala linalotia wasiwasi na Rais wa FIFA Sepp Blatter hivi karibuni amesema lilikuwa kosa kupanga kinyang'anyiro hicho cha msimu wa joto, katika taifa la jangwa.

Rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA, Michel Platini pia amethibitisha kuwa mashirkisho 54 wanachama wa UEFA wamekubaliana kwa kauli moja kuhusu wazo la kuhamisha dimba hilo la Qatar, hadi msimu mwingine wa mwaka

Lakini nayo kamati andalizi ya Qatar imejaribu kuondoa wasiwasi hiyo, kwa kusema teknolojia ya kuleta hewa ya baridi, kwa kutumia solar, katika maeneo ya umma, nje na ndani ya viwanja, huenda ikatatua shida hizo. bila shaka tutasubiri kuona jinsi namna suala hilo litakavyokwenda, nasi tutakufahamisha

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu