1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habari

Wasikilizaji na miaka 50 ya DW

16 Januari 2013

"Tangu ianzishwe, DW imetoa mchango mkubwa sana duniani kupitia habari za ulimwengu, elimu kwa jamii kuhusu afya, utamaduni na sanaa na pia kuwahusisha wasikilizaji wake kwa karibu." - Amos Msanga, Ludewa - Tanzania.

https://p.dw.com/p/17KwM
Wettbewerb zum 50-jährigem Jubiläum. Shaaban Manyanga c/o Day P.O. Box 79505 Dar es Salam, Tanzania
50 Jahre Kisuaheli Redaktion WettbewerbPicha: DW

"Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle imezidi kuwa ashiki kwangu kupitia habari zake tendeti tena zisizo mithali. Kutangamana kwangu na watangazaji wetu kupitia midahalo na makala aula nimetambulika duniani pamoja na kujenga mahusiano bora. Nimezidi kujifunza mengi tena ya umuhimu." - Kennedy Osuri, Sudan ya Kusini.

"Miaka 50 ya DW imetuhabarisha habari mbalimbali kama zile za kisiasa, michezo, utamaduni, uchumi na kadhalika." - Maulidi Fikirini, Tanzania.

"Katika kipindi cha miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle sio tu sisi wasikilizaji tumeweza kufaidika na kuelimika vyema na matangazo ya kituo hichi, lakini pia tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika muundo mzima wa DW hadi hivi sasa katika kuboresha matangazo na mfumo wa vipindi vyake hewani ili kuzidi kukidhi hamu na shauku ya wasikilizaji . Hivi sasa DW inavuma na kusikika hewani na pia tovutini katika kila pembe ya dunia yetu bila ya matatizo yoyote ya usikivu au mawasiliano." - Mubarak Ghassany, Oman.

"Asante, mie binafsi naiona DW kama mwalimu anaefundisha somo kwa umakini tena mwenye ujuzi wa kutosha. Kwanza imenitatulia tatizo la maji kijijini kwetu kupitia Jukwaa. Na mie nimeelimika kwa vipindi, Noa Bongo, na Vijana Mchaka Machaka. Ukweli DW ni bomba. Samahani kwa kuzidisha kwani uzuri wa DW mie nitasimulia hata kurasa tano. HAPPY BIRTHDAY DW!"- Riziki Barnaba, Tanzania.

"Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle ni fahari kwa wasikilizaji wake. DW imekuwa rafiki yangu wa karibu kwani ninapata elimu ya kutosha pia kuhamasika na changamoto za Maisha kupitia vipindi maridhawa na makala za kusisimua kama vile Mbiu ya Mnyonge, Sura ya Ujerumani Jukwaa la Manufaa, Afya Yako bila kusahau Noa Bongo Jenga Maisha. Binafsi nimehamasika pia nimewahamasisha wengine kuitegea sikio Idhaa ya Kiswahili ya DW." - James Mushi, Tanzania.

"Kwa mtazamo wangu, DW Kiswahili ni redio huru na isiyoufungamana na upande wowote. Imekuwa ikituhabarisha bila woga wala kificho. Nahisi hii ndiyo sifa ya kipekee inayotofautisha DW na redio zingine na hivyo kuifanya ipendwe na jamii kubwa hasa ya watu wa chini. Siku zote ukweli una nguvu kuliko uwongo. Nimejifunza mengi sana kupitia redio hii." - Gasper Mollel, Arusha - Tanzania.

"DW kweli imekuwa kivutio kikubwa sana kwangu kutokana na jinsi inavyochambua ripoti kuhusu taifa langu Kenya. Tangu nikiwa shule ya upili, nilijiwekea akiba maalum ya pesa ambazo nilikuwa napewa kama matumizi ya chakula cha mchana na nauli, mpaka ikatosha kununua redio ndogo ya mfukoni mwaka wa 1989 yaani miaka miwili kabla ya Marekani kuishambulia Iraq." - Mogire Machuki, Kisii – Kenya.

"Mwaka wa 1970 ulikuwa ni mara ya kwanza kukumbana na DW Kiswahili. Nilikuwa nimeiomba redio kutoka kwa rafiki yangu. Tangu wakati huo sikurudi nyuma kama koti bali nimekuwa mbele kama tai. Kufikia nusu ya pili ya miaka ya 1970 nilikuwa tayari nimejenga uhusiano mkubwa na DW Kiswahili kupitia mawasiliano ya barua za maoni na mashindano ya bahati nasibu. Nilipata masomo ya Kijerumani kwenye redio, vitabu na kanda. Zaidi ya hayo nilipata magazeti ya Hallo Friends na Daraja." - Bernard M. Gitahi, Nyahururu – Kenya.

"Kupitia Deutsche Welle nimeweza kuijua siasa ya Ujerumani, chaguzi, viongozi na vyama vinavyounda msimamo huo wa demokrasia iliyoiva hadi kumpata kansela mwanamke. Vyama kama CDU, CSU na The Green ni baadhi ya vyama ambavyo nimevijua kupitia redio inayopendwa ya DW. Kwa masikio yangu nimeweza kushuhudia viongozi wakubwa wa nchi ya Ujerumani kama makansela Helmut Köhl, Gerhard Schröder na sasa Mama Angela Merkel. Marais nilioshuhudia ni pamoja na Richard von Weizsacker, Johannes Rau na Hörst Köhler." - Franz Ngogo, Mara – Tanzania.

"Hakika tangu Idhaa ya Kiswahili ya DW ianzishwe imeweza kuhabarisha, kuelimisha na pia kuburudisha. Idhaa hii imeweza kuwafikia watu katika kila kona, hii ni kwa kupitia mtandao wa Intaneti katika tovuti yao. Kupitia makala zake mbalimbali ambazo zimeweza kuelimisha asilimia kubwa ya watu, hususan Afrika Mashariki." - Castory A. Anthony, Kibaha – Tanzania.

"Idhaa ya Kiswahili ya DW imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudumisha na kuendeleza uhusiano na urafiki uliopo kati ya nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili na taifa la Ujerumani. Imefanikiwa pia kurusha matangazo ambayo yamesaidia sana kuwafahamisha wananchi wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiswahili mambo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na yanayoendelea nchini Ujerumani." - Ludovick Ernest Mcharo, Arusha – Tanzania.

"Teknolojia ya upashanaji habari imetuwezesha jamii ya sasa kupata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW kupitia redio washirika za masafa ya FM zilizopo hapa nchini na kupitia tovuti kusikiliza vipindi mbalimbali pia kupokea vijarida kupitia barua pepe na kujifunza Kijerumani kupitia vipindi vya redio. Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani ni kama jirani yetu Watanzania kwa kutuunganisha pamoja kuchangia mawazo yetu katika habari za kila siku." - Jerome K. Ndubusa, Tanzania.

"Mimi ni msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW wa siku nyingi. Hongereni kwa vipindi vyenu ila muda wa vipindi hivyo ni mdogo mno. Vipindi inavyofuatilia ni vya Afya na Mazingira, kwami mimi mwenyewe ni mtayarishaji wa vipindi hivyo katika Televisheni ya Taifa la Burundi katika lugha ya Kiswahili. Ninawapongeza kwa kutimiza miaka kwani raia wengi wa nchi zinazoendelea wamefaidika kufahamu yale ambayo walikuwa hawayajui." - Masam Jumanne, Bujumbura - Burundi.

"Ambacho naishukuru DW katika miaka hii 50 na sitoweza kukisahau ni kuwa mwaka 2006 niliweza kufaulu mtihani wa darasa la saba, kwani majibu ya maswali yaliyokuja kwenye mtihani huo niliyapata kwa kusikiliza vipindi vya DW! Hongereni sana! Hivi sasa huku kwetu chakula cha mchana wamekipa jina la DW!" - Andrew Isaac Mashimba, Tegeta - Tanzania.

"Nilipata kuifahamu DW redio nikiwa mdogo sana katika miaka ya ‘90. Babu yangu mdogo kijijini kwetu ndiye peke yake aliyekuwa na redio ya mbao, kwa hiyo tulikuwa tunakwenda kwake kusikiliza vipindi vya DW redio hasa wakati wa jioni; na mpaka sasa naendelea kuisikiliza." - Julius Sajilo, Dodoma – Tanzania.

"Ninawashukuru kwa vipindi vyenu vya kuelimisha kama taarifa ya habari, haki za binaadamu, Noa Bongo, Jukwaa la Manufaa. Ninawapongeza sana kwa kazi yenu nzuri na makini kwa ulimwengu mzima. Hongereni kutimiza miaka 50." - Adam A. Mboya, Moshi – Tanzania.

"Mimi ni mmoja wa wasikilizaji wenu watiifu kwa miaka 40 sasa. Ninaendelea kuitegemea DW kwani imebakia kuwa redio pekee inayotoa taarifa za habari za kuaminika kwa miaka 50 iliyopita. Makala ya Wanawake ni kizuri sana katika kuwaelimisha wanawake juu ya masuala mbalimbali tusiyojua kuwa ni haki yetu." - Fatuma Miraji, Sikonge – Tanzania.

"Tangu mwaka 1990, nilianza kuwaona wazee hapa visiwani wakisikiliza, na kutoka hapo nikawa nafadika kujua mengi yanayotokea duniani. DW inatoa elimu ya bure na binafsi napenda makala za mazingira, taarifa za habari na kozi ya Kijerumani. Kutokana na makala zenu za mazingira, nimeanzisha mradi wangu mwenyewe wa kupanda miti na kozi ya Kijerumani inaniwezesha kufanya kazi na wanafunzi na watalii kutoka Ujerumani." - Iss-haka Hussein Abdulla, Zanzibar - Tanzania.

"Ninawapongeza kwa kipindi kizuri kipya cha Kinagaubaga kilichoanza hivi karibuni. Safari ya kipindi imeanza Kenya na kufuatiwa na Zanzibar na tumepata kusikia kutoka kwa wahusika wenyewe. Naiombea demokrasia ikite mizizi kwenye mataifa hayo." - Arthur Kabugu, Mtapwa, Mombasa - Kenya.

"Shukurani nyingi kwa DW na redio washirika. Kupitia vipindi munavyotangaza, tunajifunza mengi. Kwa redio washirika wanaorusha matangazo yenu, ningeliwaomba kwamba waongeze muda wa matangazo ya DW, na isiwe nusu tu, bali yote mazima." - Robert Thomas, Tabora – Tanzania.

"Mimi ni msikilizaji mzuri wa vipindi mbalimbali vya DW. Nimekuwa nikifuatilia mara kwa mara kipindi cha wanawake na maendeleo cha DW. Kwa hakika kipindi hiki huandaliwa kwa umakini na mada zake huwa za kusisimua sana napenda niwapongeze waandaaji wa kipindi hiki. Nimevutiwa sana na mada ya ukeketaji iliyorushwa hewani hivi karibuni, hata hivyo si kwa kuifurahia mila hiyo bali kuipinga na kuikemea vikali." - Henry Kideula, Njombe – Tanzania.

Tanbihi: Haya ni maoni mbalimbali ya wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW. Picha imechorwa na Shaaban Manyanga wa Dar es Salaam, Tanzania, kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya DW.


Mhariri: Mohammed Khelef