1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana 82 wa Chibok waachiwa huru na Boko Haram

Caro Robi
7 Mei 2017

Serikali ya Nigeria imesema wasichana 82 wa waliotekwa nyara na waasi wa Boko Haram miaka mitatu iliyopita wameachiwa huru na katika makubaliano ya kuwaachia huru wafungwa wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Boko Haram.

https://p.dw.com/p/2cXgA
Nigeria Chibok-Mädchen in Abuja
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Aghaeze/

Ofisi ya Rais imetangaza miezi kadhaa ya mazungumzo na majihadi hao yamezaa matunda miezi sita baada ya wasichana wengine 21 kuachiwa huru na Boko Haram. Hata hivyo hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu idadi ya washukiwa wanachama wa kundi hilo la waasi walioachiwa huru.

Wasichana hao walioachiwa huru watasafirishwa hadi mji mkuu wa Nigeria, Abuja Jumapili ili kukutana na Rais Muhamadu Buhari. Rais Buhari ameishukuru serikali ya Uswisi, Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu na mashirika kadhaa ya kimataifa na ya Nigeria yasiyokuwa ya serikali kwa kusadia katika kuaachiwa huru kwa wasichana hao wa Chibok.

Kuachiwa kwa wasichana wa Chibok kwaibua matumaini

Duru za kijeshi na za kiraia katika mji wa Banki ulioko mpakani kati ya Nigeria na Cameroon zimearifu kuwa takriban wasichana 80 walifikishwa mjini humo Jumamosi adhuhuri na kupelekwa katika kambi za kijeshi.

Screenshot mutmaßliches Boko Haram Video
Baadhi ya wasichana wa Chibok waliotekwa na Boko HaramPicha: youtube/Fgghhfc Ffhjjj

Seneta wa Nigeria Shehu Sani ambaye alihusika katika mazungumzo ya awali ya kuachiwa huru kwa wasichana hao amesema wengi wao wako katika hali nzuri ya afya. Serikali imesema inafanya kila juhidi kuhakikisha wasichana wengine wa Chibok ambao bado wako mikononi mwa waasi hao wanaachiwa huru.

Boko Haram waliivamia shule ya wasichana ya sekondari katika mji wa Chibok mnamo tarehe 14 Aprili 2014 na kuwateka nyara wasichana 276 waliokuwa wanajiandaa kufanya mitihani yao ya kitaifa. 57 kati yao walifanikiwa kutoroka lakini 219 walizuiwa na kundi hilo.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau aliyeapa kuwasilimisha na kuwaoza wasichana hao wa Chibok katika kipindi hca nyuma alisema wasichana hao wataachiwa huru iwapo serikali ya Nigeria itawaachia huru wapiganaji wake wanaouzuiwa.

Siku ya Ijumaa, Uingereza na Marekani zilionya kuwa Boko Haram inapanga kuwateka nyara raia wa kigeni katika eneo la Banki, hatua iliyosababisha kusitishwa shughuli ya kupeleka misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Sudi Mnette