1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yakosolewa kuhusu ukandamizaji wa vyombo vya habari

3 Novemba 2015

Washirika wa Uturuki kutoka Magharibi wameelezea wasiwasi wao kutokana na vitisho vilivyotolewa na serikali ya nchi hiyo kwa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi wa bunge uliokirejesha madarakani chama cha Rais Erdogan.

https://p.dw.com/p/1Gyid
Rais Recep Tayyip Erdogan
Rais Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Waangalizi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE, wamesema uchaguzi huo umefanyika huku kukiwa na mazingira ya hofu. Mkuu wa timu ya waangalizi wa OSCE, Ignacio Sanchez Amor, amesema pia kuna wasiwasi mkubwa kwamba waandishi wa habari walikuwa katika shinikizo wakati wa kampeni.

''Changamoto ya usalama imeshuhudiwa hasa katika eneo la kusini-mashariki ikiwemo matukio kadhaa ya ghasia na mashambulizi dhidi ya wafuasi wa vyama, hali iliyowazuia wagombea kuendesha kampeni kwa uhuru,'' alisisitiza Amor.

Wakosoaji wameonya kuhusu suala la kuwepo dalili za udiktekta kwenye nchi hiyo ambayo tayari imegawanyika. Chama cha Rais Recep Tayyip Erdogan cha Haki na Maendeleo-AKP kimeshinda katika uchaguzi wa bunge ambao uliitishwa mapema na uliofanyika siku ya Jumapili, na hivyo kuirejesha madarakani serikali ya chama kimoja.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Josh Earnest
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Josh EarnestPicha: picture alliance / AP Images

Mbali na OSCE, Marekani ambayo ni mshirika muhimu wa Uturuki, imesema ina wasiwasi kuhusu ukandamizaji uliokuwa unafanywa dhidi ya vyombo vya habari vinavyomkosoa Rais Erdogan.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Josh Earnest amesema wana wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza kwa ujumla, pamoja na uhuru wa kukusanyika, nchini Uturuki.

PACE nayo yatoa maoni yake

Kwa upande wake, mkuu wa timu ya waangalizi kutoka Bunge la Baraza la Ulaya-PACE, Andreas Gross amesema kwa bahati mbaya kampeni za uchaguzi huo hazikuwa za haki na ziligubikwa na hofu.

Akizungumza jana Erdogan, aliutolea wito ulimwengu kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo wa bunge. Hata hivyo, ushindi wa Erdogan unazusha maswali mengi kuhusu chama chake cha AKP kupata wingi wa viti bungeni, miezi mitano baada ya kuupoteza wingi huo kutokana na ushindani mkali wa chama cha mrengo wa kushoto kinachowaunga mkono Wakurdi cha HDP, ambacho kwenye uchaguzi wa sasa kimepata zaidi ya asilimia 10 ya kura zilizopigwa.

Vitisho kwa waandishi wa habari viliendelea hapo jana, baada ya kukamatwa kwa mhariri wa jarida la Istanbul la Nokta, baada ya kuandika ripoti iliyopewa kichwa cha habari: ''Mwanzo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Uturuki.'' Jarida hilo limeshutumiwa kwa kuuchochea umma kufanya uhalifu.

Maafisa wa HDP, Ali Haydar Konca na Muslum Dogan
Maafisa wa HDP, Ali Haydar Konca na Muslum DoganPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Wakati huo huo, polisi nchini Uturuki leo imewakamata watu 35, wakiwemo watendaji waandamizi wa serikali na maafisa wa polisi, kama sehemu ya kuwachunguza wafuasi wa kiongozi wa kidini wa Uturuki mwenye makaazi yake nchini Marekani, anayetuhumiwa kupanga njama za kumuangusha Rais Erdogan.

Fethullah Gulen, anayeishi uhamishoni Marekani na aliyekuwa mshirika wa Erdogan na kisha kugeuka kuwa adui yake kutokana na juhudi za mhubiri huyo kutaka kuingia madarakani, anatuhumiwa kwa kuendesha kundi la kigaidi na kesi yake inatarajiwa kusikilizwa mwezi Januari, bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Daniel Gakuba