1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Wabunge wa chama cha Democratic wafurahia kujiuzulu kwa Rove

14 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZI

Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wamefurahia kujiuzulu kwa mshauri wa rais George W Bush, Karl Rove.

Karl Rove ametangaza atajiuzulu mwishoni mwa mwezi huu akisema anataka kuwa na muda zaidi na familia yake huko Texas.

Mgombea urais wa chama cha Democtratic, John Edwards, amesema ni afadhali kwamba Rove ameondoka.

Naye seneta Barack Obama, ambaye pia atagombea urais wa Marekani mwakani, amesema mkakatiwa kisiasa wa Karl Rove umeicha Marekani ikiwa imegawanyika, masilahi ya kibinafsi yakipewa kipaumbele na Wamarekani wakiachwa nje na serikali yao katika historia ya nchi hiyo.

Akizungumza baada ya kujiuzulu Karl Rove, rais Bush amesema wamekuwa marafiki kwa muda mrefu na wataendelea kubakia marafiki.

´Tumekuwa marafiki kwa muda mrefu na tutaendelea kuwa marafiki. Naweza kumuita Karl Rove kuwa rafiki yangu wa karibu sana. Tumefahamiana kama vijana tuliokuwa na ari ya kulitumikia taifa letu, kufanya kazi pamoja ili kuweza kuwa katika nafasi ya kuitumikia nchi hii. Kwa hiyo namshukuru sana rafiki yangu kwa kujitolea kwa dhati na nakutakia kila la heri.´

Gazeti moja mashuhuri nchini Marekani limekueleza kujiuzulu kwa mtaalamu huyo wa maswala ya kisiasa katika ikulu ya Marekani kuwa mchezo mbaya.

Gazeti la New York Times toleo la leo limewataka wabunge wa Marekani wachunguze jukumu la Karl Rove katika visa vya kufutwa kazi waongozaji mashtaka kadhaa wa serikali na juhudi zake za kuchanganya siasa na maswala ya serikali mjini Washington.