1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Gates akanusha kutaka kuishambulia Iran

16 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCRo

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesisitiza kwamba Ikulu ya Marekani haitafuti kisingizio cha kuanzisha vita dhidi ya Iran.

Katika wiki za hivi karibuni utawala wa Rais George W. Bush umezidisha shinikizo kwa Iran kwa kuishutumu kuchochea machafuko nchini Iraq kwa kuwapatia wanamgambo wa kimadhehebu silaha zilizotengenezwa nchini Iran.Nancy Pelosi ambaye ni mbunge wa upinzani wa chama cha Demokratik na spika wa Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani amesema Rais Bush hana madaraka katika bunge ya kumuwezesha kuanzisha vita Iran.

Pelosi alikuwa akizungumza katika siku ya tatu mfululizo ya mjadala juu ya azimio lisiloshurutisha lenye kupinga nia ya Bush ya kuongeza wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanya na Kituo cha Utafiti cha Pew unaonyesha kwamba asilimia 53 ya Wamarekani wanaamini kwamba Marekani inapaswa kuwarudisha nyumbani wanajeshi wake.